Home Uncategorized HAYA MADUDU YANAYOENDELEA NDANI YA LIGI KUU BARA NA LIGI DARAJA LA...

HAYA MADUDU YANAYOENDELEA NDANI YA LIGI KUU BARA NA LIGI DARAJA LA KWANZA YASIFUMBIWE MACHO

BADO kuna mambo ambayo yanaendelea kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi Daraja la Kwanza yanafurahisha na kuumiza pia wakati mwingine kutokana na namna ambavyo yanatokea huku wahusika wakiwa kimya kama hakuna kitu ambacho kimetokea.
Huku kwenye Ligi Daraja la Kwanza picha inayoendelea kwa sasa ni vita kwa timu kutafuta nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara jambo ambalo linafanya kila mmoja akomae kupata matokeo.
Kumekuwa na kasumba ya timu wenyeji kutamba kupata matokeo kwa namna yoyote kutoka kwa wapinzani wao jambo ambalo linahitaji umakini mkubwa.
Timu nyingi zimekuwa zikitumia kivuli cha kuwa nyumbani kufanya visa na kusahau kwamba maisha ya soka ni mzunguko ambao huwezi kuukwepa kwa namna yoyote yule utakayemfanyia ubaya leo kesho utakutana naye.
Tambo hizi zilianza kwa timu nyingi ila zilikwama kufikia mafanikio kutokana na falsafa ya mpira kuwakataa wababe na kuwakubali wale ambao wanacheza soka kwa kufuata sheria 17.
Achana na wale wababe pia wapo wale ambao walionja  joto ya kwenye ligi waliposhuka kwa sasa mambo yao yanakwenda kombo yote ukianza kufuatilia utagundua kwamba walipanda kwa njia ambazo hazikuwa na mashiko.
Hakuna timu inayopanda kwa magumashi ikaweza kudumu ndani ya ligi lazima itashushwa na maisha yataendelea ila kwa zile ambazo zilipanda kwa uhalali na kushushwa kimagumashi bado nafasi yao imeshikiliwa kwa muda wajipe moyo mkuu watarejea.
Kuna zile ambazo zinalia na ukata kuna umuhimu kwao kutafuta vyanzo vitakavyowapa mshiko kabla ya kuanza kutembeza bakuli kuomba sapoti hakuna ambaye anafikiria shida ya mtu mwingine ambaye hajaanza kuonesha nia ya kujinasua pale alipo.
Njombe Mji timu ya wilayani Njombe inahaha kupata wadhamini hapo kuna ulazima wa kuangalia mbinu mpya zitakazoweza kuwanusuru viongozi pamoja na timu kiujumla isiposhtuka utashangaa inashuka Ligi Daraja la Kwanza na kuibukia Daraja la Pili huko.
Tukirudi kwenye Ligi Kuu Bara kuna matukio ambayo yana mwendelezo yanafurahisha na kukasirisha kutokana na wahusika wenyewe kujitambua na kuwa sehemu ambayo wanapaswa kuwa mfano.
Mfululizo wa wachezaji wa timu moja kucheza mchezo isiyo ya kiuungwana na timu yenyewe falsafa yake ikiwa inaegemea kwenye nguvu moja hapa kuna tatizo limejificha ila hawataki kuweka wazi.
Naizungumzia Simba ambayo ilimpiga chini Kocha Mkuu Patrick Aussems kwa kueleza kuwa alishindwa kusimamia nidhamu na wakati huu kumekuwa na mwendelezo wa matukio ambayo hayafurahishi.
Haina maana kwamba wakati wa Aussems wachezaji walikuwa hawafanyi matukio ya kipuuzi hapana nakumbuka ilikuwa kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara Uwanja wa Nangwanda Sijaona msimu uliopita, Erasto Nyoni alikutana na balaa la Kamati ya Masaa 72 kwa kosa la kumchezea rafu mchezaji wa Ndanda.
Msimu huu Simba ikiwa chini ya Mbelgiji Sven Vandenbroeck, wachezaji wamekuwa wakionekana wakifanya vitendo visivyo vya kinidhamu na hakuna hatua ambayo Simba inachukua juu yao maisha yanaendelea kwa wachezaji kupeta ndani ya Uwanja bila neno lolote.
Hili sio sawa likiendelea linatibua taswira ya Simba ambayo ilianza kujijenga kuwa ya kimataifa kwa namna inavyokwenda kila siku inarudi hatua tano nyuma kabla ya kushuhudia anguko kwa kushindwa kuthibiti nidhamu ya wachezaji.
Pascal Wawa, Jonas Mkude na Clatosu Chama hawa ni nyota wenye uzoefu lakini yale wanayowafanyia wachezaji wenzao ndani ya Uwanja yanashusha thamani yao, Simba, wachezaji lazima wabadilike.

SOMA NA HII  AZAM FC LEO KUTESTI MITAMBO NA MASHINE HIZI MPYA KALI KINOMA