Home Uncategorized TUUNGANE KWA PAMOJA KUPAMBANA NA CORONA, WACHEZAJI MKIBWETEKA MNAJIDANGANYA WENYEWE

TUUNGANE KWA PAMOJA KUPAMBANA NA CORONA, WACHEZAJI MKIBWETEKA MNAJIDANGANYA WENYEWE

NI wazi inafahamika kwa sasa ligi mbalimbali duniani zimesimama ikiwa ni sehemu ya kujikinga zaidi na maambukizi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.
Tangu kusimama kwa ligi hizo ikiwemo ya Tanzania, zimepita zaidi ya siku kumi, hivi sasa wachezaji wanafanya mazoezi binafsi kutokana na program walizopewa na makocha wao.
Wakati huu wa mapumziko ya ligi, wachezaji wamepata likizo ambayo hawakuitarajia na kujikuta wakiwa nje ya sehemu zao za kazi kwa kubakia nyumbani.
Wakiwa nyumbani madaktari mbalimbali wametoa namna bora ya kufanya mazoezi kwa kipindi hiki hata kama hausimamiwi na kocha au kiongozi wako yeyote yule.
Sasa kwa wachezaji wengine licha ya kwamba wamepewa programu hizo lakini hawazifuati jambo ambalo siyo zuri hata kidogo kwa sababu mazoezi ambayo wamepewa ni kwa ajili ya wao binafsi.
Haitapendeza kuona mchezaji anarudi klabuni kwake na kupimwa kisha kuonekana alikaa tu nyumbani bila ya kufanya jitihada ya mazoezi yoyote yale.
Mchezaji unatakiwa kutambua kwamba soka ndiyo kazi yako, hivyo kufanya udanganyifu ni kosa kubwa sana.
Kumbuka kama umepewa program ya kufanya halafu wewe hufanyi, humdanganyi kocha wala mtu mwingine, bali unajidanganya mwenyewe.
Kocha akiona umerudi katika timu halafu haupo kwenye kiwango anachokitaka ni wazi atakuweka nje, hapo hasara inakuwa kwako.
Wachezaji fuateni kile ambacho mnaambiwa na makocha wenu hasa katika kufuata program mlizoachiwa. Likizo hii ya ghafla isiwafanye mkabweteka.
Kuna timu hivi sasa katika Ligi Kuu Bara zinapambana kwa nafasi ilizonazo.
Zipo ambazo zinawania ubingwa kama Simba, Yanga na Azam ingawa Simba ndiyo ipo karibu sana katika kuchukua ubingwa.
Zingine zipo chini zikihangaika kujinasua na janga la kushuka daraja kama Singida United, Mbao, Alliance, Mbeya City, Ndanda na Mwadui.
Sasa wachezaji wa timu hizo zote nilizozibainisha kama wakibweteka itakuwa hasara kwao na timu kwa jumla kwani zitashindwa kufikia malengo.
Kwa zinazohangaika kujinasua kushuka daraja, zinaweza kushuka kutokana na wachezaji wao kufanya uzembe wakati huu walipopata mapumziko.
Lakini zile zinazowania ubingwa, nazo zinaweza kukosa kama wachezaji watashindwa kufanya kile ambacho makocha wao wanawaelekeza.
Ujanjaujanja kazini haufai, popote pale ukiweka ujanjaujanja mbele zaidi ya kufanya kazi kwa usahihi lazima utafeli.
Waliofanikiwa wote wamekuwa wakifanya kazi kwa usahihi wakifuata yale yanayotakiwa. Ukiona mtu amefeli lakini anafuata kanuni alizopewa, basi fuatilia lazima kuna sehemu hafanyi kwa usahihi.
Wachezaji jitambueni, kipindi hiki fanyeni mazoezi lakini pia mkiendelea kujilinda juu ya Virusi vya Corona.
Tutambue kwamba virusi hivi ni hatari, watu duniani wamekuwa wakifariki kila siku na maambukizi nayo yamekuwa yakiongezeka kwa baadhi ya nchi.
Kila mmoja wetu kwa nafasi yake lazima achukue tahadhari. Serikali inaelekeza namna ya kujikinga na virusi hivi, hivyo tusikilize kwa umakini maelekezo na kuyafuata.
Tuungane kwa pamoja kuvitokomeza Virusi hivi vinasumbua dunia kwa sasa. Kama tukivitokomeza ni wazi michezo itarudi tena kama zamani.
Hivi sasa hakuna michezo, wanamichezo tunapata shida sana, lakini Corona ndiyo chanzo cha yote, hatuna budi kuipiga vita.
SOMA NA HII  RAIS MAGUFULI AUMIZWA NA KUONDOKA KWA MUGABE, ATOA TAMKO