Home Uncategorized KAGERA WATIA NGUMU MAXIME KUTUA YANGA

KAGERA WATIA NGUMU MAXIME KUTUA YANGA

BAADA ya kuwapo kwa tetesi za Yanga kuendelea kumwania Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime, uongozi wa timu hiyo umesema kocha wake haendi kokote, imefahamika.

Inaelezwa kuwa Januari 15 mwaka huu, siku ambayo Yanga iliikaribisha Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara, ilimpatia Maxime (pichani) nakala ya mkataba, ambao hadi kufikia jana nahodha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa (Taifa Stars), hajausaini.

Kiongozi mmoja wa juu wa Kagera Sugar aliliambia gazeti hili kuwa tayari wameshaboresha maslahi ya Maxime na wanaamini ataendelea kubakia katika klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba, mkoani Kagera.

“Tunajua katika maisha kuna kuangalia maslahi, kwa kuzingatia hilo, tumeshauboresha mkataba wake wa awali na naweza kusema hata ofa ya Yanga ilikuwa haitofautiani sana na mshahara na bonasi anayolipwa hapa kwetu,” alisema kiongozi huyo.

Aliongeza Kagera Sugar imekuwa ikiwalipa vema wachezaji na waajiriwa wengine, hivyo uamuzi wa mtu kuondoka hautatokana na kigezo cha maslahi pekee.

Katika mchezo huo wa Januari 15, Kagera Sugar iliwachapa Yanga mabao 3-0, matokeo ambayo yaliendelea kuwatoa kwenye mbio za ubingwa.

SOMA NA HII  STRAIKA HUYU ATAFUNGA SANA, MWAMNYETO ATOA KAULI YA KIBABE, NDANI YA CHAMPIONI JUMAMOSI