Home Uncategorized KUHUSU BILIONI 20 ZA MO NDANI YA SIMBA..A-Z YA MCHAKATO UPO HIZI

KUHUSU BILIONI 20 ZA MO NDANI YA SIMBA..A-Z YA MCHAKATO UPO HIZI

KAMATI ya kuratibu mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu ya Simba imesema kuwa wanachama watalazimika kusubiri hadi miezi minne (siku 120) ili mchakato wa mabadiliko mfumo huo uanze rasmi. Lakini mambo yakishaanza, Simba itatingisha kwelikweli Tanzania na nje ya mipaka.

Klabu ya Simba ilianza mchakato wa kufanya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji takribani miaka miwili na nusu iliyopita baada ya kufanya utafiti na mfumo wa sasa hautaiwezesha klabu hiyo kupata maendeleo.

Katika mchakato huo wa mabadiliko ya mfumo, mwekezaji, Mohammed ‘Mo’ Dewji kupitia kampuni ya Mo Simba Holding Limited itawekeza Sh 20 bilioni kwa ajili ya hisa 49 huku wanachama kupitia kwa wadhamini wa klabu hiyo watawakilishwa kupitia kampuni ya Simba Holding Limited ikimiliki hisa 51.

Mmoja wa wajumbe wa kamati inayosimamia mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo, Mulamu Nghambi alisema kuwa mpaka sasa klabu ya Simba imekwisha sajili kampuni yake, Simba Holding Limited ambayo inamilikiwa na wanachama.

Mbali ya Nghambi wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Aziz Kefile ambaye ni mwenyekiti, Arnold Kashembe (Katibu wa Kamati ambaye pia ni mkurugenzi wa uendeshaji wa Simba), Barbara Gonzalez, Haroub Suleiman, Mwina Kaduguda ambaye pia ndiyo kaimu mwenyekiti wa Klabu ya Simba na wanasheria wa klabu wakiongonzwa na Michael Mhina na Evodius Mtawala.

Mjumbe Nghambi alisema kuwa kwa mujibu wa taratibu, kampuni hiyo imesajiliwa Brela na ni mali ya wanachama wa klabu hiyo huku mwekezaji, Mo’ Dewji naye amekwisha kamilisha usajili wa kampuni ambayo itawekeza ndani ya klabu hiyo ijulikanayo kwa jina la Mo Simba Holding Limited.

Vile vile Nghambi amesema kuwa ; “Kampuni ambayo itaendesha klabu ya Simba, Simba Sports Club Limited nayo imekwisha sajiliwa tayari kwa kuanza kazi pamoja na kusubiri utaratibu za kisheria ambazo zinatupasa kuwasilisha baadhi ya nyaraka hizo kwenye Tume ya Ushindani (FCC) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukamilisha taratibu kwa mujibu wa kisheria.”

Alifafanua kuwa sheria ya FCC inawalazimu kusubiri siku120 ili kujiridhisha na utaratibu uliotumika ili timu hiyo ianze mfumo mpya wa uendeshaji.

“Mpaka sasa kampuni zote zote zimesajiliwa na sasa tunaelekea kwenye utaratibu wa mwisho ambao utatulazimu kusubiri kipindi hicho, taratibu za FCC zimeweka muda huo, lakini unaweza kupungua kutokana na wao kujiridhisha na maelezo kutoka kwetu maana hili ni jambo jipya na la kwanza kwa klabu kufanya mabadiliko ya uendeshaji,

SOMA NA HII  HIKI NDICHO ALICHOKIFANYA KAPOMBE, MORRISON ALITIBUA, KESHO NDANI YA CHAMPIONI JUMATATU

Ukisikia klabu au taasisi imekamilisha mfumo wa uendeshaji lazima uipongeze kwani una taratibu nyingi za kufuatwa za kisheria mpaka kufanikisha, kwa sasa Simba ipo katika hatua ya mwisho na tunaamini tutafanikiwa,” alisema Nghambi.

Kwa upande wa TRA, Nghambi alisema; “Kimsingi, tumefikia hatua nzuri na hakuna ucheleweshwaji wa mchakato huu, hata timu nyingine ambazo zina mpango wa kuanza mfumo mpya wa uendeshaji, italazimika kufuata utaratibu uliowekwa, hakuna njia ya mkato.”

BILIONI 20 ZA UWEKEZAJI

Nghambi alisema kuwa kwa sasa ni vigumu kwa mwekezaji kupitia kampuni yake ya Mo Simba Holding Limited kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya Simba Sports Club Limited kutokana na kutokukamilika kwa taratibu mbali mbali.

Alisema kuwa wanamshukuru sana Mo Dewji kwani ameonyesha moyo wa kiungwana kwa kuamua kufungua akaunti maalum na kuweka fedha hizo pamoja na kuwa zoezi kuwa bado kutokana na taratibu za nchi.

Amesema kuwa Mo ameamua kuweka fedha hizo kwenye akaunti ya muda maalum ili klabu iweze kujiendesha.

Nghambi alisema kuwa mbali ya fedha za wadhamini wao mbalimbali, hatua ya Mo kuwekeza fedha hizo kwenye akaunti ya muda maalum inaiwezesha timu kupata Sh bilioni 1.6 kwa mwaka.

Mo pia anatoa udhamini wa Sh milioni 250 kinywaji cha Mo Extra na Sh 150 milioni kupitia Mo Halisi na kuifanya jumla ya Sh 2 billioni kwa mwaka.Alisema kuwa kwa sasa Simba imeanza kufaidika na mchakato huo pamoja na kutofikia hatua za mwisho kwa mwekezaji kujenga viwanja viwili vya mazoezi maeno ya Bunju Dar es Salaam.

“Mo amefanya hivi ili kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kwani mpaka sasa Simba imeweza kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo na kushiriki katika mashindano ya kimataifa,

“Pindi zoezi litakapokamilika, mwekezaji atakuwa katika hatua nzuri kwani atakuwa anawekeza kwenye klabu ambayo tayari ina mafanikio na kazi itakayokuwa imebaki ni kuendeleza yale ambayo yalikuwa hayafanyiki kutokana na taratibu za kisheria,” alisema Nghambi.