Home Uncategorized MO DEWJI ANOGESHA SHOO SIMBA

MO DEWJI ANOGESHA SHOO SIMBA

MAMBO ni moto ndani ya klabu ya Simba kwa wakati huu ambao wanaonekana wazi kukaribia kuupokea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wekundu wa Msimbazi hao, Mohammed Dewji ‘Mo’, akizidi kukoleza shamra shamra hizo.

Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City juzi kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, Simba walijiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo, wakihitaji pointi mbili tu kubeba ‘mwali’.

Na wanapojiandaa kuivaa Tanzania Prisons kwenye uwanja huo Jumapili, Wekundu wa Msimbazi hao wanaonekana kuwa na matumaini makubwa ya kutoka na ushindi na kuanza sherehe za ubingwa jijini Mbeya.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Simba ipo kileleni ikiwa na pointi 78 ilizozivuna kutokana na mechi 31, huku ikisaliwa na michezo saba, wakati nafasi ya pili inashikiliwa na Azam yenye pointi 58 na Yanga wakiwa wa tatu na pointi zao 56.

Na iwapo Simba itaichapa Tanzania Prisons katika mchezo wao wa Jumapili, itakuwa imetangaza ubingwa kwa kufikisha pointi 81 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote.

Kwa kufahamu hilo, Mo Dewji ameposti ujumbe uliozidi kuwapandisha mzuka Wanamsimbazi uliosomeka: “Mpira umeisha pointi tatu muhimu. Hongera benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla! Msimu huu unadhani tutakabidhiwa kombe lini?”

Mo Dewji ameposti hujumbe huo kama sehemu ya kuonyesha kuwa ni wazi Simba ndiye bingwa wa Ligi Kuu Bara na kilichobaki ni kukabidhiwa kombe tu.

Tayari ujumbe huo wa Mo Dewji umewaibuka mabosi wa benchi la ufundi la Simba alilolipongeza, likiongozwa na Sven Vandenbroeck na msaidizi wake, Seleman Matola ambao wamewataka mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo popote walipo, kumiminika Mbeya kuanza sherehe za ubingwa.

Akizungumza na BINGWA jana kutoka Mbeya, Matola aliwataka mashabiki wao kujitokeza kwa wingi katika mchezo wao na Tanzania Prisons kuwashudia vijana wao wakiandika historia ya kuchukua ubingwa mara ya tatu mfululizo.

Matola alisema amefurahishwa na mwitikio wa wapenzi wao waliohudhuria mechi yao iliyopita akiamini walichangia kwa kiasi kikubwa ushindi wao dhidi ya Mbeya City, akihitaji ‘nyomi’ zaidi Jumapili.

“Niwapongeze Wanasimba waliojitokeza kwa wingi kuwapa sapoti wachezaji, ninachowaambia hatutawaangusha, tutafanya kile wanachotamani, naomba waje tena kwa wingi kutupa sapoti Jumapili,” alisema Matola.

Akizungumzia mchezo wao na Mbeya City, Matola alisema wachezaji wao walifanya walichowaelekeza muda mfupi kabla ya mechi kutokana na hali waliyokutana nayo Mbeya.

“Wachezaji wameweza kufanya kile tulichowatuma, imekuwa ni ngumu kwetu kutokana na uwanja haukuwa mzuri na kutufanya kucheza mpira ambao hatujauzoea, lakini niwapongeze wachezaji wamepambana,” alisema.

Naye nahodha wa kikosi hicho, John Bocco ambaye ndiye mfungaji wa mabao yote mawili dhidi ya Mbeya City, alisema siri kubwa ya kile wanachokifanya ni ushirikiano na umoja waliokuwa nao wachezaji.

“Tumejitolea kila mchezaji kupata ushindi huu, ninachofurahia tunacheza kwa ushirikiano mkubwa na kutufanya tuwe na kiwango kizuri, tunaelekeza nguvu zetu mchezo ujao,” alisema Bocco.

Mshambuliaji huyo alisema hawatabweteka na ushindi wao wa juzi wanapoelekea kuivaa Tanzania Prisons, wakiwa wamejipanga kucheza kila mechi kwa kujituma hadi dakika ya mwisho hadi watakapotwaa ubingwa.

SOMA NA HII  BUKAYO SAKA AONGEZA DILI REFU NDANI YA ARSENAL