Home Uncategorized KIUNGO WA SIMBA ATIBUA DILI LA NYOTA WA RWANDA KUTUA YANGA

KIUNGO WA SIMBA ATIBUA DILI LA NYOTA WA RWANDA KUTUA YANGA


JAMES Kotei, kiungo wa zamani wa Simba anatajwa kuingia kwenye rada za mabosi wa Yanga kwa ajili ya kumpa dili la kukitumikia kikosi hicho kwa msimu wa 2020/21.

Iwapo nyota huyo dili lake litakamilika litapeperusha dili la Ally Niyonzima ambaye pia alikuwa kwenye rada za timu hiyo.
Ally Niyonzima anakipiga katika Klabu ya Rayon Sports na timu ya taifa ya Rwanda, katika timu hizo amekuwa akitumika kama kiungo mshambuliaji na mkabaji kutokana na uwezo mkubwa alionao.
Taarifa kutoka kwa chanzo  cha kuaminika, zinasema Niyonzima alikuwa kwenye mipango ya kusajiliwa na Yanga kutokana na kupendekezwa na Kocha Luc Eymael, lakini viongozi hawamhitaji yeye bali wanamhitaji Kotei ambaye aliwahi kuonyesha ubora wake akiwa anaitumikia Simba.
“Ally Niyonzima alikuwa kwenye mazungumzo na Yanga kwa muda mrefu na aliahidiwa baada ya kumalizika kwa mchezo wa nusu fainali ya FA dhidi ya Simba watamalizana naye, lakini viongozi walimfungia vioo kabisa.

“Kocha Luc Eymael alimpendekeza Niyonzima na inaonekana alikuwa anamhitaji zaidi, lakini viongozi wengi wa Yanga hawamtaki yeye, bali wanamtaka Kotei kwani wanaamini atawasaidia sana kama alivyoisaidia Simba,” kilisema chanzo chetu.

Baada ya Spoti Xtra kuzipata taarifa hizo, lilimtafuta mchezaji huyo kuzungumzia dili lake na Yanga, lakini hakuwa tayari kuzungumza chochote, huku viongozi wa Yanga wakiomba waachwe kwanza hadi kipindi cha usajili kifike ndiyo watazungumza zaidi.
Ikumbukwe kuwa, Kotei alijiunga na Simba Desemba 2016, akaondoka Juni 2019. Kwa muda aliokaa ndani ya Simba, ameshinda Kombe la Shirikisho la Azam, Ligi Kuu Bara mara mbili, huku akiifikisha Simba robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
SOMA NA HII  SALAMBA: NINAPATA USHIRIKIANO MZURI KWA WENZANGU