Home Uncategorized MASHABIKI WA SIMBA KUPIGA PICHA BURE NA KOMBE NI HASARA

MASHABIKI WA SIMBA KUPIGA PICHA BURE NA KOMBE NI HASARA



NA SALEH ALLY
WASWAHILI wanasema tembea uone, hakuna asiyelijua hili na kama umewahi kutembea, basi utagundua mgaagaa na upwa hali wali mkavu.

HUu ukavu si lazima kupata fedha, inawezekana kabisa ukapata jambo ambalo likawa muhimu na vigumu kulinuna kwa fedha. Ninaaminisha ukajifunza na kuwa bora zaidi.

Nimekumbuka kuzungumza nanyi wadau baada ya kuona klabu ya Simba ikiwa inawakaribisha mashabiki wake waende kwa wingi katika mechi yao dhidi ya Alliance kwenye Uwanja wa Taifa, jana.

Mechi hiyo ilikuwa ni ya mwisho kwa Simba kwa msimu huu kucheza kwenye Uwanja wa Taifa katika mechi za Ligi Kuu Bara. 

Nafikiri ni wazo zuri, mashabiki wana haki ya kusherekea ubingwa wa kikosi chao ambacho walipambana nacho pamoja kwa muda wote hadi kufikia mafanikio kwa kuwa wao ndio walikuwa nguvu ya kikosi chenyewe kukipa nguvu.

Pamoja na hivyo, binafsi naona kitendo cha mashabiki hao kwenda kupiga picha na kombe hilo, hakukuwa na ubunifu zaidi na ubunifu sahihi, badala yake jambo hilo likafanyika kwa mazoea, ndio maana nasema ni hasara kubwa kwa kwa klabu ya Simba.

Mashabiki ndio wanaozifanya timu kuwa na fedha nyingi na Tajiri na si vinginevyo. Na ili wawe maada na kutumika vizuri lazima wale wanaokuwa katika klabu, mfano Simba wawe wabunifu wa hali ya juu kuweza kuwatumia mashabiki kuifanya klabu kubwa na nguvu sana kwa maana ya fedha, umaarufu na kadhalika.

Kwanza, huwa ni uwanjani, kuendelea kuwa na ubinifu kuwaita mashabiki uwanjani kwa ushawishi mkubwa kabisa. Wanapokwenda uwanjani kwa wingi, faida zinajulikana. Moja ni kuipa nguvu timu ifanye vizuri dhidi ya wapinzani lakini pili, viingilio ambavyo ni mapato ya klabu.

Klabu inapokuwa na kipato kikubwa, maana yake inaweza kufanya mambo yake kwa wakati na usahihi na majibu ya hapa ni kutengeneza utajiri na ukubwa.

Simba wamelichukulia jambo la kupiga picha kama shukurani, lakini Real Madrid, FC Barcelona, Arsenal, Manchester United, Liverpool, Everton na wengine wamelichukulia suala hilo kuwa ni biashara na mashabiki wanapata nafasi ya kufurahi lakini klabu ikiwa imeongeza nguvu kwa kuingiza fedha.

Mara nyingine nimewaelezea nilivyojifunza kupitia safari nyingi kwenda kuhoji au kujifunza kupitia wenzetu barani Ulaya karibu kila sehemu nililipia kuyaona makombe ya klabu hizo kubwa nilizozitaja hapo juu na nyingine.

Makombe utayaona lakini lazima ulipie na wakati mwingine unalipa hadi zaid ya Sh 100,000 kwa kupita katika jumba maalum ambalo kuna makombe na kumbukumbu nyingine za klabu hiyo ambazo zimepatikana kwa muda wote.

Mfano, Simba kwa sasa wangekuwa wanatangaza kuwa watu wajitokeze nah ii si pale uwanjani, badala yake lingekuwa tukio maalum la kwenda kupiga picha na wachezaji na kombe hilo. 

Wakati wa upigaji picha, ukipiga halafu unasubiri kwa dakika 5, picha yako inatoka na unalipia. Picha inayotoka inakuwa na nembo ya Simba ikiwezekana na zile za wadhamini.

Shabiki atahifadhi picha hiyo kwa kumbukumbu na atailipia angalau kwa Sh 1,500 tu. Jiulize kama mashabiki watajitokeza 50,000 maana yake itaingiza Sh milioni 75 katika zoezi hilo. 

Inawezekana kabisa kama zoezi litafanyika nchi nzima, maana yake Simba inaweza kuingiza hadi zaidi ya Sh milioni 500. Kazi hii ikifanyika kwa ubunifu, wachezaji wakishirikishwa hata kama ni baadhi au kwa makundi kwa mkoa na mkoa, lingekuwa jambo la faida na mbolea kwa Simba.

Haya mambo wakati mwingine yanaonekana ni madogo, kiasi cha fedha kama Sh 1,500 kinaweza kudharaulika lakini kiuhalisia, kidogo ndio kinchotengeneza kikubwa na hapa viongozi Simba wajifunze kwa kuwa mashabiki kutoa Sh 1,500 kwa ajili ya kombe la ubingwa na kukiwa na utaratibu mzuri, hakuna atakayeona ni hasara maana ndio furaha yao.

Nawakumbuka, mashabiki ni faida lakini lazima kuwe na akili ya ziada.



SOMA NA HII  HIKI NDCHO KINACHOMPA KIBURI EYMAEL KUSEPA NA POINTI TATU ZA MBEYA CITY