Home Uncategorized KMC YAENDELEZA DOZI, YAISHUSHA AZAM FC NAFASI YA KWANZA

KMC YAENDELEZA DOZI, YAISHUSHA AZAM FC NAFASI YA KWANZA

KLABU ya KMC wana Kino Boys leo wamendelea na rekodi yao ya kushinda mechi za Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Mwadui FC.

Ushindi huo unaifanya KMC kusepa na pointi tatu na kuishusha Azam FC nafasi ya kwanza baada ya kufikisha pointi 9 ikiwa imetupia jumla ya mabao 10 na imefungwa mabao mawili ndani ya dakika 270.


Azam FC inakuwa nafasi ya pili na pointi zao 9 kwa idadi ya mabao ya kushinda ambapo Azam FC imefunga mabao manne msimu wa 2020/21. 

Mchezo wa leo uliochezwa Uwanja wa Mwadui Complex ulikuwa ni wa tatu kwa KMC kushinda huku ukiwa ni wa tatu kwa Mwadui FC kupoteza ndani ya msimu wa 2020/21.

Relliants Lusajo, ingizo jipya ndani ya KMC aliyeibukia huko akitokea Klabu ya Namungo amepachika mabao yote mawili ikiwa ni dakika ya 75 na 84 kipindi cha pili baada ya ngoma kuwa ngumu dakika 45 za kipindi cha kwanza kwao.

Licha ya Mwadui FC kuwa ya kwanza kuitungua KMC dakika ya 11 kupitia kwa nyota wao Issa Shaban ngoma ilikuwa nzito kwao kusepa na pointi tatu mazima.

KMC ilianza mchezo wake wa kwanza mbele ya Mbeya City kwa kushinda mabao 4-0 kisha ikamalizana na Tanzania Prisons kwa ushindi wa mabao 2-1 na leo imemalizana na Mwadui FC kwa ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ni mchezo wake wa kwanza ugenini.


Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema kuwa walijipanga kufanya vizuri na wanaamini wataendelea kutua burudani kwa mashabiki na wadau wa KMC. 


SOMA NA HII  AZAM FC NGUVU ZOTE SASA KWA MBAO FC