Home Uncategorized MASHABIKI TUENDELEE KUJITOKEZA UWANJANI KUZIPA SAPOTI TIMU

MASHABIKI TUENDELEE KUJITOKEZA UWANJANI KUZIPA SAPOTI TIMU

 


MSIMU wa Ligi Kuu Bara 2020/21 unazidi  kushika kasi na kupamba vichwa vya habari kila  kukicha kutokana na upinzani mkubwa wa timu 18 zinazoshiriki ambazo bila shaka zimethibitisha kuwa zilijipanga vyema.

 

  Licha timu zote kuwa na muda mchache wa maandalizi uliopelekewa na mabadiliko ya ratiba kufuatia janga la maambukizi ya Virusi vya Corona bado kuna ushindani unaonekana ndani ya uwanja.

 

Ligi ya msimu huu imekuwa na msisimko mkubwa kutokana na ushindani mkubwa ambao umekuwa ukionekana katika michezo mbalimbali ambayo tayari imepigwa mpaka sasa.

 

 Wachezaji wamekuwa wakipambana kuonyesha uwezo wao ndani ya uwanja na ni jambo la msingi linalotakiwa kwa kuwa kazi yao ni kucheza na kutafuta matokeo kwenye mechi zote.

 

Ushindani ndani ya ligi ya msimu huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na usajili ambao umefanyika kwenye kila klabu inayoshiriki msimu huu.

 

Tumetoka kupita kwenye kipindi cha usajili ambacho kilifungwa Agosti 31, baada ya kufunguliwa Agosti Mosi na timu nyingi zilionekana kuingia sokoni kusaka wachezaji waliokuwa wakiwahitaji.

 

Suala jingine ambalo limewavutia na labda kuwashangaza watu wengi ni namna ambavyo ushindani wa namba umekuwa mkubwa miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na wale ambao walikuwa ndani ya vikosi hivyo msimu uliopita.

 

Tayari tumeshuhudia baadhi ya nyota ambao walikuwa wamejihakikishia nafasi ya kuanza kwenye vikosi vya kwanza msimu uliopita wakiwa wanapata wakati mgumu kupata nafasi ya kuingia kwenye vikosi vikosi vyao msimu huu.

 

Ushindani ule wa kweli unahitajika kwa kuwa ili timu ipate kushinda ni lazima iwe na wachezaji makini na wenye uwezo ambao wanaweza kuipa timu matokeo.

 

Kila wakati ndani ya ligi kunapaswa kuwe na ushindani kuanzia mwanzo mpaka mwisho hii itaongeza thamani ya ligi pamoja na mchezaji mwenyewe ndani ya uwanja.

 

Licha ya ushindani wa ligi ya msimu ambao umeendelea kuonekana kwa kipindi cha majuma matatu yaliyochezwa mpaka sasa lakini nadhani bado kuna changamoto kubwa ya maamuzi ambayo yamekuwa yakifanywa na waamuzi wetu.

 

Kila mmoja ni shahidi wa namna ambavyo baadhi ya waaamuzi msimu uliopita walivyoingia matatani na kusababisha malalamiko makubwa kutokana na maamuzi ya utata waliyoyafanya ambapo hata baadhi yao kujikuta wakipata adhabu ya kufungiwa kutochezesha michezo kadhaa.

 

Adhabu za msimu uliopita kujirudia tena wakati huu ni mbaya na haitapendeza kwa kuwa kuna wakati wa kujifunza na ule wa kufanya makosa tayari umepita.

 

Baadhi ya mechi zilizochezwa hivi karibuni zimeanza kulalamikiwa na mashabiki pamoja na wadau wa mpira huu sio mwanza mzuri katika hili.

SOMA NA HII  MWALIMU MKUU ATUHUMIWA KUBAKA, KUMPA MIMBA MWANAFUNZI, ASOMEWA MASHTAKA SABA

 

Imeripotiwa kwamba kwenye mchezo wa ligi uliowakutanisha Mbeya City dhidi ya Azama FC hapa kuna maofisa wa mechi pamoja na waamuzi wa mchezo huo walitolewa uwanjani wakiwa chini ya uangalizi wa Polisi.

Suala hili ni baya na linaleta picha mbaya hasa kwa soka letu ambalo kwa sasa linafuatiliwa zaidi na wengi kutoka ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

Katika hili Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) linapaswa liangalie upya na kwa ukaribu namna bora itakayowafanya waamuzi kuweza kufuata sheria 17 za soka.

Tukiachana na masuala ya waamuzi ningependa pia kwa uchache kugusia kwa kupongeza kuhusiana na mwamko mkubwa wa mashabiki wa soka hapa nchini ambao wamekuwa wakizidi kuwa na mapenzi makubwa na mchezo wa soka kila kukicha.

 

Ni muhimu hamasa hizi zikaendelea kuongezeka kwani kwa kufanya hivyo mashabiki wengi zaidi watahamasika kujitokeza uwanjani kuzishuhudia timu zao ambapo kiujumla mapato yatakayopatikana kupitia viingilio vyao yanaweza kuzisaidia timu zao kujiendesha kiuchumi.

 

Lakini pia viongozi wa mashabiki kwenye matawi mbalimbali hapa nchini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wenzao ili kusapoti miradi mbalimbali ya klabu kama vile ununuaji wa jezi orijino za klabu zao.

 

Kwa namna ya pekee pia nawapongeza wadhamini mbalimbali ambao wanaendelea kujitokeza kuungana na TFF ili kuongeza nguvu katika kuipa thamani ligi ya msimu huu kwa kuchangia kiasi cha fedha za udhamini.

 

Pia nawapongeza Azam Tv ambao wamekuwa wakirusha matangazo ya michezo moja kwa moja yaani ‘mubashara’ kwa kiwango kinachovutia.

 

Kupitia matangazo hayo si tu kwamba Watanzania ambao hawana nafasi ya kuingia uwanjani nao wanapata burudani kupitia matangazo ya televisheni lakini pia wapenzi wa soka wanapata nafasi ya kujifunza mengi kuhusu mchezo huo.

 

 Lakini hata kwa waamuzi na kamati ya nidhamu wanapata nafasi ya kufanya maamuzi kupitia faida za marejeo ya rekodi za video.

 Hawatazamin Bongo pekee bali mpaka nje ya nchi kuna watu ambao wanaifuatilia ligi yetu hivyo ni fursa kwa wachezaji kuweza kujiweka sokoni kwa ajili ya wakati ujao.

Kwa wachezaji ambao wanashindwa kuendelea kuwa wabunifu ndani ya uwanja wanapaswa wajifunze kupitia wale ambao wanafanya vizuri.

Muda bado kwa sasa ligi ndo inaanza kinachotakiwa kwa timu zote ni kujipanga vizuri ili kupata matokeo chanya ambayo yatawafanya wafikie malengo ambayo wamejiwekea.