Home Uncategorized OKTOBA INA MENGI KINOMA, SIMBA YALAMBISHWA SHUBIRI

OKTOBA INA MENGI KINOMA, SIMBA YALAMBISHWA SHUBIRI


 NI hesabu za vidole tu ambazo unaweza kuzifanya wakati ambao unataka kuubadilisha mwezi Oktoba kwenda ule unaofuata wa Novemba. Huu ni mwezi wapili wa mwisho wa mwaka.

Mwezi Oktoba unaondoka ukiwa na mambo mengi kuanzia ya kijamii, siasa na hata muziki. Kama umesahau nakukumbusha leo Jumatano ndiyo Watanzania wanapiga kura kuchagua marais, wabunge na madiwani.

Pia mwezi huu katika upande wa soka hasa Ligi Kuu Bara umekuwa na vingi ambavyo vimeacha alama zake ambapo makala haya yanakukumbusha yaliyotokea kwenye mwezi huo.

 

Cedric Kaze atua, asaini Yanga

Baada ya kumkosa mwanzoni mwa msimu mabosi wa Yanga walimtangaza Mrundi Cedric Kaze kuwa kocha wao mkuu akichukua mikoba ya Mserbia Zlatko Krmpotić aliyesitishiwa mkataba wake.

Kaze alitua nchini Oktoba 15 na moja kwa moja kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu hiyo na kwenye mechi yake ya kwanza akashinda kwa bao 1-0.


Oktoba 3, wakati timu yake ikishinda mabao 3-0 mbele ya Coastal Union Uwanja wa Mkapa ilikuwa ni kete yake ya mwisho kisha akachimbishwa.

 

Simba yalambishwa shubiri

Oktoba inaisha vibaya kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba baada ya kukutana na kipigo cha kwanza kwa msimu huu. Hiyo ilikuwa Oktoba 22 ambapo walifungwa bao 1-0 na Tanzania Prisons katika Uwanja wa Nelson Mandela, Rukwa.

Hiki kilikuwa kipigo cha kwanza kwa jeshi hilo la Simba ambalo lilicheza mechi tano bila ya kufungwa hata mechi moja.

 

Eeeh! Simba na Yanga yapepea        

Kwa mwezi huu wa Oktoba imeyeyuka mechi kubwa kwa hapa Tanzania. Ndiyo ni mechi ya watani wa jadi, Yanga ambao walikuwa wenyeji wa Simba kwenye Kariakoo Dabi.

Mzigo ulikuwa upigwe Oktoba 18, lakini ikasogezwa mbele na sasa utapigwa Novemba 7 pale kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.

   

Maka, Amri Said waliwa vichwa

Makocha wawili, Amri Said wa Mbeya City na Maka Mwalwisi aliyekuwa Ihefu SC hawawezi kuusahau mwezi Oktoba kwani uliwafanya waondolewe kwenye sehemu zao za kazi.

SOMA NA HII  MRITHI WA ARISTICA CIOABA HUYU HAPA APEWA MECHI MBILI

Maka ndiye aliyeanza Oktoba 6 kisha Amri akafuata Oktoba 20, wote mwezi huu kamwe hauwezi kuwa mzuri hata kidogo.

 

Katwila apakimbia Mtibwa, aibuka Ihefu

Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubeir Katwila aliwashangaza wengi baada ya kuikimbia klabu hiyo na kutimkia sehemu kwingine.

Baada ya kubwaga manyanga Mtibwa Sugar siku si nyingi kwa maana Oktoba 18, Katwila akaibukia Mbeya katika Klabu ya Ihefu SC akiwa ndiye kocha mkuu.

  

Mbeya City waona nyota

Mbeya City kwa mwezi huu wana historia nao kwani walifukuza kocha na wakapata ushindi wao wa kwanza ndani ya mwezi huu.

Baada ya kuwa na siku ngumu za mwezi Septemba na za mwanzoni mwa Oktoba, Mbeya City wakaonja radha ya ushindi Oktoba 25 baada ya kuwachapa Kagera Sugar mabao 2-0. Mbeya City ilibidi wasubiri mechi za Oktoba 20 dhidi ya Mwadui, Oktoba 16 mbele Dodoma Jiji na Oktoba Mosi dhidi ya Prisons ambazo zote hawakushinda.