Home Uncategorized MAMBO YAWE MAPYA NDANI YA 2021

MAMBO YAWE MAPYA NDANI YA 2021


 YALE ambayo yalikuwa ni matatizo kwa mwaka 2020 basi inapaswa yawekwe kando na kutafutiwa majibu yake ndani ya 2021 kwa kuwa sasa ni mwaka mpya na yale ya kale yamepita ndani ya ulimwengu wa michezo.

Taratibu Januari inaanza kumeguka kuifukuzia Februari kabla ya kuibukia Machi ikiwa ni kasi ya kuyeyusha siku zilizopo ndani ya mwaka huu mpya 2021.

Kikubwa ambacho ninaamini ni kwamba makosa yote yanaachwa mwaka uliopita na mwaka huu mpya utakuwa ni mwaka wa majibu ya yale maswali magumu yalikuwa yakiulizwa mwaka uliopita.

Kuanzia kwa waamuzi namna ambayo walikuwa wakiamua ndani ya uwanja, sasa ni mwanzo mpya ndani ya 2021 kwa kufanya vizuri zaidi na kujibu yale maswali ya mwaka uliopita.

Hakuna haja ya kuanza kurudia makosa na kuboronga zaidi kama ilivyokuwa mwaka ulioisha hapana. Inawezekana kufanya vema kwa kuwa ni mwanzo mpya katika kurekebisha makosa ambayo yamepita.

Sheria 17 za mpira kwa sasa ni muhimu kufuatwa zaidi kwa waamuzi. Kutazama namna ambayo itakuwa bora katika kutimiza utaratibu kuliko kuchezesha soka letu kwa mazoea.

Hakuna mafanikio ikiwa mazoea yatatawala ndani ya Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza na la Pili bila kusahau Ligi ya Wanawake Bongo ni lazima kufanya yote kwa weledi ndani ya uwanja.

Hakuna timu ambayo inapenda kushuka daraja hivyo matokeo mabovu ndani ya uwanja nayo pia yaachwe mwaka uliopita. Inawezekana kwa sasa kujipanga upya na kufanya vizuri.

Timu zile ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja zina kazi ya kupambana kusaka matokeo chanya ndani ya uwanja.

Ninaona kwamba zipo ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka jumla hata kabla ya mechi za Ligi Kuu Bara hazijaisha kwa sasa ndani ya ligi.

Kinachotakiwa kwa sasa ni kubadili gia ile ya mwanzo iliyokuwa ikitumika mwaka uliopita na kuja na gia nyingine ambayo itakuwa na matokeo mazuri.

Ipo wazi kwamba kila timu ndani ya uwanja ina uwezo wa kupata matokeo yale ambayo inahitaji ndani ya uwanja na kuweka kando yale yaliyopita.

SOMA NA HII  CORONA IMEFUTA LIGI ZA NCHI HIZI HAPA MSIMU WA 2019/20

Wachezaji mitazamo ya mwaka uliopita tupa kule kwa sasa ni muhimu kuja na mtazamo mpya kwa kuwa mwaka ni mpya na mambo yanapaswa kuwa mapya.

Benchi la ufundi zile mbinu za 87 ambazo zimekuwa zikitumiwa kusaka matokeo nazo zisipewe nafasi kwani zimeonekana kushindwa kutoa matokeo chanya ndani ya uwanja.

Kikubwa kinachotakiwa ni kuleta mipango kazi upya ambayo itaweza kuleta ushindani upya kama ambavyo tunaufungua ukurasa mwingine.

Ikiwa timu ama wachezaji watashindwa kwenda na kasi mpya ndani ya mwaka huu basi tutarajie anguko kwa baadhi ya timu huku waamuzi nao pia wakikutana na lile rungu la kufungiwa kazi zao.

Kila la kheri ndani ya mwaka mpya wawakilishi wetu kimataifa, Simba ikiwa mtatumia akili za mwaka uliopita kwamba Uwanja wa Mkapa ni machinjio mtaambulia maumivu, lazima mtambue kwamba mpo nyumbani ila mnatakiwa kucheza na sio kuamini mtashinda.

Namungo ugenini kila la kheri mkamalize upya kazi mliyoanza kuifanya Uwanja wa Azam Complex.