Home CAF NAMUNGO KAZI KWENU LEO KUPEPERUSHA BENDERA KIMATAIFA

NAMUNGO KAZI KWENU LEO KUPEPERUSHA BENDERA KIMATAIFA

 


NGOMA itakayochezwa leo Uwanja wa Mkapa ni kati ya Namungo FC ya Ruangwa dhidi ya Nkana FC ya Zambia kwenye mchezo wa makundi Kombe la Shirikisho.

Kubwa ambalo linapaswa kufanyika kwa Namungo ni kuweza kupambana na kuonja ushindi wao wa kwanza kwenye Kombe la Shirikisho, hatua ya makundi.

Ilikuwa ni ngumu kwenye mechi zilizopita kwa kuwa mbili zote imepoteza na kuambulia maumivu kwenye mechi hizo zilizokuwa na ushindani.

Ile ya kwanza ambayo ilichezwa ugenini ilikuwa ngumu kwa Namungo kupata ushindi licha ya kupambana kufikia lengo hilo mwisho ilipoteza na kuambulia maumivu mbele ya Raja Casablanca.

Ule wa pili ilipokuwa nyumbani pia ilishindwa kuambulia ushindi kwa sababu ilipoteza ikiwa nyumbani, haya ni maumivu na ngoma inaonekana ilikuwa nzito kwa wote dhidi ya Pyramids.

Leo inawezekana kupata ushindi ikiwa kila mchezaji atajituma na kufanyia kazi yale makosa ambayo wamekuwa wakiyafanya kwenye mechi zao zilizopita.

Ipo wazi kwamba mchezo wa mpira ni mchezo wa makosa lakini kuna kuyatumia makosa ya wapinzani kupata matokeo chanya na maisha yakaendelea.

Kila Mtanzania anaamini kwamba Namungo ina wachezaji wazuri na wanaweza kuipeperusha bendera ya Tanzania katika kusaka ushindi.

Muda uliopo wa kurejesha matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali ni leo kwani kwa sasa mechi ambazo zimebaki ikiwa itashinda angalau itarejesha morali kwa wachezaji pamoja na timu kiujumla kurudi kwenye ubora.

Habari njema ni kwamba kuwa nyumbani ni furaha na kila mchezaji anapaswa kujivunia hilo. Kila mmoja anapenda kuona timu inapata matokeo chanya na inawezekana ikiwa mtaamua kujituma.

Tumeona kwamba jana ilikuwa Simba wao waliwakaribisha AS Vita na matokeo yao hayana uwezo wa kubadilika yatabaki kuwa hivyohivyo daima.

Ushindi wao wa mabao 4-1 mbele ya AS Vita iwe chachu kwenu pia kuendelea kuwapa fraha mashabiki.


Hivyo iwe darasa pia kwa Namungo kwamba matokeo ambayo watayapata leo hawataweza kuyabadili ikiwa watapata matokeo mazuri ama mabaya yatabaki hivyohivyo.

SOMA NA HII  KOMBE LA SHIRIKISHO: NAMUNGO 0-3 RAJA CASABLANCA

Mbinu za mwalimu ambazo zimepangwa basi zitumike huku wachezaji nao waongeze juhudi kwa kutumia na mbinu zao pale mambo ambapo yanakuwa magumu.

Kushindwa kupata matokeo wakati mwingine imekuwa ikisababishwa na wachezaji kushindwa kutumia nafasi ambazo wanazitengeneza uwanjani.

Inawezekana kupata ushindi kwa wachezaji ambao wataanza kutumia nafasi vizuri zile ambazo watazipata bila kukosea.

Ni mara chache kupata nafasi kwenye mechi za kimataifa na kushindwa kuzitumia kurudi hizo nafasi huwa inakuwa ngumu.

Basi kinachotakiwa leo wachezaji kwa pamoja kuwa watulivu kuanzia ile safu ya ulinzi mpaka ushambuliaji kwa sababu ni kazi ya Tanzania.

Vita ya dakika 90 na timu ambazo hazina pointi huwa inapendeza ikiwa mwenyeji atashinda akishindwa basi maumivu huwa yanakuwa makubwa.

Basi kwa sababu deni lipo, wachezaji pambaneni kulipa deni kwa mashabiki na ipo nafasi ya kurekebisha makosa ambayo mmeyafanya wakati uliopita.

Kila la kheri Namungo, dua za Watanzania zipo kwenu na imani kubwa ni kwamba mtapata matokeo chanya na pointi zenu mtaweka kibindoni.