Home Ligi Kuu HIZI HAPA ZILIPOTEZA MECHI CHACHE 2020/21 VPL

HIZI HAPA ZILIPOTEZA MECHI CHACHE 2020/21 VPL


MSIMU mpya wa 2021/22 upo karibu kuanza huku joto kwa kila timu likizidi kupanda kwa kuwa hakuna anayejua nani atakuwa nani kwa msimu mpya unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku zile timu ambazo zilipoteza kwa kufungwa mechi chache nazo zikiwa hazijapata picha namna hali itakavyokuwa.

Hapa leo tunakwenda kutazama timu tano ambazo zilipoteza mechi chache ndani ya uwanja kwa msimu wa 2020/21 baada ya kila timu kucheza jumla ya mechi 34 ambazo ni dakika 3,060.

Namba moja ipo mikononi mwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ambayo yenyewe kwa msimu mzima iliambulia kichapo kwenye mechi mbili pekee kati ya 34 na ilifungwa mbele ya Coastal Union ya Tanga, ubao wa Uwanja wa Mkwakwani ulisoma Coastal Union 2-1 Yanga.

Mchezo wa pili kwa Yanga kufungwa ilikuwa mbele ya Azam FC mpachikaji wa bao alikuwa ni muuaji anayetabasamu Prince Dube ambaye alipachika bao hilo akiwa nje ya 18, Uwanja wa Mkapa ukasoma Yanga 0-1 Azam FC.

Pia Yanga ilimaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kukusanya jumla ya pointi 74 inakibarua cha kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021/22.

Namba mbili ni Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes ambayo yenyewe iliambulia kichapo kwenye mechi tatu, ile mechi ya kwanza kupoteza ilikuwa mbele ya Wajelajela, Tanzania Prisons na lilipigwa pira gwaride kwa timu hiyo kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 huko Songea.

Mchezo wa pili Simba kunyooshwa ilichezeshwa tena pira gwaride na Ruvu Shooting, Uwanja wa Uhuru pale Dar es Salaam ngoma ilikamilika, Simba 0-1 Ruvu Shooting na ule wa tatu walinyooshwa na watani zao wa jadi Yanga, Uwanja wa Mkapa bao 1-0.

Licha ya kupoteza mechi hizo tatu, Simba iliweza kutetea taji la Ligi Kuu Bara na ina kibarua kingine kwa msimu wa 2021/22 cha kuona namna gani itatetea taji hilo.

Timu namba tatu kwa kufungwa mechi chache ni Azam FC ambayo ilipoteza jumla ya mechi nne na mchezo wake wa kwanza kutunguliwa ilikuwa mbele ya Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri, Moro mji kasoro bahari.

SOMA NA HII  MSIMAMO WA LIGI KUU BARA UPO NAMNA HII

Namba nne ambayo ilipoteza mechi chache ni Polisi Tanzania inayonolewa na Malale Hamsini na ilipoteza jumla ya mechi 9 pekee ambazo ni sawa na dakika 810 ilimaliza ikiwa nafasi ya 6 na pointi zake kibindoni ni 45.

Namba tano ipo mikononi mwa timu mbili kwa kuwa zote zilimaliza msimu kwa kufungwa mechi 10 pekee kati ya 34 ni Biashara United ya Mara wanajiita Wanajeshi wa mpakani na ilimaliza ikiwa nafasi ya 4 na pointi zake ni 50 na nyingine Tanzania Prisons ilimaliza ikiwa nafasi ya 7 na pointi 44.