Home Habari za michezo KISA AL MAREKH GAMONDI AMPA DOZI MAALUM MAXI

KISA AL MAREKH GAMONDI AMPA DOZI MAALUM MAXI

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi raia wa Argentina, ameamua kuwapeleka ufukweni wachezaji wote wa kikosi hicho akiwemo Maxi Nzengeli ikiwa ni maandalizi ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan.

Yanga ambayo imeanza msimu huu kwa mafanikio kutokana na kutoa vipigo vizito katika Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika, Septemba 16, mwaka huu inatarajiwa kuwa ugenini kupambana na Al Merrikh ukiwa ni mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya kwanza.

Baada ya mchezo huo ambao umepangwa kupigwa nchini Rwanda, timu hizo zinatarajiwa kurudiana Dar, Septemba 30, mwaka huu. Mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo, huku atakayepoteza, safari itaishia hapo kwa msimu huu.

Kocha huyo ambaye anaonekana amepania kuweka rekodi ya Yanga kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, juzi aliwapeleka wachezaji wa timu hiyo gym katika viwanja vya Gymkhana, huku akipanga kesho Jumatatu kuwapeleka Ufukwe wa Coco kwa ajili ya kujenga stamina zaidi.

Gamondi ameliambia Spoti Xtra kwamba, hawatakuwa na muda wa kupumzika zaidi ya siku za wikiendi pekee kwa kuwa mikakati yake ni kujenga timu imara itakayoshindana na kupata matokeo bora wakati wowote.

“Wachezaji ninawapumzisha siku mbili, Jumamosi na Jumapili, Jumatatu asubuhi tutafanya mazoezi ufukweni kwa ajili ya kuongeza stamina katika miili ya wachezaji wangu.

“Safari yetu iliyo mbele ni kubwa, hatuhitaji kukaa kusubiria ratiba zifikie ndiyo turudi kujipanga, tunachokiangalia ni kwa jinsi gani tunaweza kupata matokeo mazuri kwa kuhakikisha timu yetu inakuwa imara muda wote ndiyo maana ratiba zetu tunaendelea, hatujasimama,” alisema Gamondi.

Gamondi amechukua hatua hiyo ikiwa Ligi Kuu Bara imesimama kwa takribani wiki mbili kupisha ratiba ya mechi za timu za taifa kufuzu AFCON.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YAO YA LIGI...GEITA GOLD WAICHIMBA MKWARA WA 'KISUKUMA' SIMBA...