Home Habari za michezo MUDATHIR AGEUKA MWIBA HUKO LIGI KUU

MUDATHIR AGEUKA MWIBA HUKO LIGI KUU

Habari za Yanga

Timu yoyote itakayocheza na Yanga kisha kuona kiungo Mudathir Yahya akianzia benchi, kisha akaingizwa kwa mabadiliko, basi lazima ijipange kwani huyo jamaa ana balaa na hasa timu hiyo inapocheza Uwanja wa Azam Complex, alipojitangazia ufalme kimyakimya.

Mudathir aliyewahi kutamba na Azam FC na Singida United, juzi aliingia uwanjani na kufunga bao pekee lililoipa Yanga ushindi mbele ya Namungo katika mechi ya Ligi Kuu Bara, likiwa ni moja kati ya mabao muhimu ambayo kiungo huyo amekuwa akiifungia timu hiyo kwenye michuano mbalimbali.

Kiungo huyo aliingia kuchukua nafasi ya Clement Mzize wakati timu hizo zikiwa hazijafungana, kisha kufunga bao hilo dakika ya 88 akimalizia pasi ya Kouassi Yao aliyeuwahi mpira wa Stephane Aziz KI uliompita tobo beki wa Namungo na baada ya mchezo huo kutamba ana ufalme wake Azam Complex.

Hilo lilikuwa bao la tatu kwa kiungo huyo katika mechi za Ligi Kuu Bara tangu ajiunge na timu hiyo kwenye dirisha dogo lililopita, lakini mabao yake yakiwa ni muhimu na kuipa pointi tatu timu hiyo, mbali na bao aliloitungua TP Mazembe iliyokufa 3-1 katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita.

Mudathir aliyeitumikia kwa mafanikio Azam FC inayoumiliki uwanja huo kabla ya kutimka misimu miwili iliyopita huwa na balaa akitokea kwenye benchi aliifungia timu yake mabao muhimu yakipindua matokeo ya mchezo, lakini aking’ara zaidi kwenye uwanja huo aliozoea kwa muda mrefu.

YANGA v DODOMA JIJI

Msimu uliopita Mudathir aliwahi kufanya kitu kama hicho akitokea benchi wakati Yanga ikiwa mwenyeji wa Dodoma Jiji Azam Complex ambapo akitokea benchi.

Kwenye mchezo huo Mudathir aliitoa timu yake nyuma kwa mabao 2-1 akiisawazishia bao la dakika ya 70 kwa shuti la mguu wa kushoto akipokea pasi ya Mzize aliyetangulia kugongeana vizuri na Farid Mussa.

Hakuishia hapo akaja kufunga bao la nne lililoihakikishia Yanga ushindi akimchambua beki na kumgeuza ndani ya eneo la hatari kisha kufunga kwa shuti tena la mguu wa kushoto akimalizia pasi ya mshambuliaji wa zamani, Fiston Mayele na Yanga ikitangaza ubingwa wa ligi kwa ushindi wa mabaio 4-2.

Juzi amerudia tena ubabe wake huo ndani ya uwanja huo akitokea benchi dakika ya 68 mechi ikionekana kuwa ngumu akatumia dakika 20 kuihakikishia ushindi timu yake akifunga bao safi la mguu wa kulia akimalizia krosi ya beki wake wa kulia Yao Kouassi.

AOGA NOTI

Baada ya mchezo huo kumalizika Mudathir alijikuta akimwagiwa fedha na vigogo wa klabu hiyo walioketi jukwaa kuu wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji wakifurahishwa na ushindi huo wa bao lake.

HUYU HAPA

Akizungumzia mabao hayo Mudathir amedai uwanja wa Chamazi ni mali yake alisema akiwa anatokea benchi hupokea maelekezo ya makocha wake katika kuubadilisha mchezo kwa jinsi upungufu aliouona.

“Kwanza niseme huu ni uwanja wangu naujua lakini wakati naingia kocha aliniambia niubadilishe mchezo huo, aliniambia jinsi wapinzani wetu walivyokuwa wanacheza wengi nyuma wakicheza mpira wa kupaki basi,” alisema Mudathir aliyefichua staili ya kushangilia kwa kuonyesha ishara ya kupiga simu kwa ajili ya watoto wake.

“Akaniambia nikiingia mpira ukiwa pembeni basi nikae nyuma ya mabeki wao alafu ikipigwa krosi nichomoke na kufunga na hilo likafanikiwa, unajua ni vigumu sana kucheza na timu inayokupa nafasi ya kuuchezea mpira alafu wao wakapaki basi.”

SOMA NA HII  KWANI MMENUNA