Home Habari za Yanga Leo GAMONDI WALA HANA PRESHA NA UTATU PACHA CPA YANGA

GAMONDI WALA HANA PRESHA NA UTATU PACHA CPA YANGA

HABARI ZA YANGA

MASHABIKI wana Presha kuhusu usajili wa Mastaa kibao kwenye kikosi chao,  haswa ule utatu pacha uliopewa jina la CPA, kwa maana ya Chama, Pacome na Aziz Ki hata hivyo, tofauti na presha za mashabiki, kwa Miguel Gamondi mambo ni tofauti kama alivyozungumza akiwasifu wachezaji wote wa kikosi hicho.

Akizungumzia usajili huo Gamondi alisema tofauti na wengine wanavyofikiri akisisitiza kwamba wala hana presha yoyote zaidi ya kufurahia aina ya kazi ambayo imefanywa na viongozi wake.

Gamondi ambaye msimu uliopita alichukua mataji mawili makubwa ya ndani, sambamba na kuifikisha Yanga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema kwa sasa ana jeshi kamili litakalokuwa na uamuzi wake aanze na nani.

Kocha huyo raia wa Argentina alisema, presha itakuwa kwa wachezaji wenyewe kwani wanatakiwa kupambana kuanzia mazoezini hadi katika mechi ili afanye uamuzi wa kuanza na nani kisha nani atokee benchi.

“Ki ukweli najibu tena, sina presha kabisa yaani sina kabisa, kwangu nafurahia tu ujio wa wachezaji bora kama hawa tunategemea watajituma ili Yanga ifanikiwe, labda presha itakuwa kwao itategemea nani anajituma kuanzia mazoezini hadi kwenye mechi,” alisema Gamondi na kuongeza;

“Unajua tupo hapa kuhakikisha tunafikia malengo yetu, tunataka kufika mbali zaidi kwenye mashindano makubwa ya Afrika, malengo kama haya lazima uwe na kikosi chenye hadhi kubwa kama hiki na kila mmoja wetu kujituma eneo lake.

“Nina furaha kwa kuwa tuna timu kubwa, viongozi wamefanya kazi kubwa kuwabakisha wachezaji tuliowataka na kupata wale bora wapya sasa tutaamua uanze na nani aanzie benchi, msimu uliopita kuna eneo tulipata shida, tunafahamu haitakuwa rahisi kila timu imejipanga lakini msimu ujao tutakuwa imara zaidi, tutapambana na yoyote.

Yanga inaendelea kujifua kenye kambi iliyopo Avic Town, Kigamboni jijini Dar es Salaam kabka ya kwenda Afrika Kusini kushiriki michuano maalumu ya Toyota Cup na Agosti 4 itatambulisha jeshi zima la msimu wa 2024-2025 katika Kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi kabla ya siku nne baadae kuvaana na Simba katika Dabi ya kwanza ya Ngao ya Jamii , ikirejea fainali ya msimu uliopita na kulala kwa penalti 3-1 jijini Tanga.

SOMA NA HII  ALLY KAMWE:- TUMETOKA LAKINI TUNA REKODI ZETU....ANAYESEMA TUMEKIMBIA AJE TUKIPIGE..