Home Habari za Simba Leo SIMBA YAVIUNGO IMERUDI…WAPINZANI MJIANDAE

SIMBA YAVIUNGO IMERUDI…WAPINZANI MJIANDAE

HABARI ZA SIMBA

Usajili wa Augustine Okejepha kutoka Rivers United kuja Simba unaashiria kazi ngumu iliyopo mbele ya kocha mpya wa timu hiyo, Fadru Davids katika upangaji wa timu yake msimu ujao.

Okejepha anajiunga na Simba kuchukua nafasi ya kiungo aliyedumu kwa miezi 6 tu kalbuni hapo Babacar Sarr ambaye timu hiyo itampa Thank You kutokana na kutoridhishwa na kiwango alichoonyesha msimu uliopita.

“Ni rasmi tumekamilisha usajili wa kiungo mkabaji Augustine Okajepha raia wa Nigeria kutoka Rivers United kwa mkataba wa miaka mitatu. Okejepha ni mchezaji kijana mwenye umri wa miaka 20 aliyetunukiwa kipaji kikubwa katika idara ya kiungo wa ulinzi.

“Katika miaka kadhaa sasa tumekuwa tukihitaji kupata mchezaji ambaye ataipa uimara safu yetu ya ulinzi na Okajepha anatarajiwa kuwa suluhisho. Okejepha ndiye mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu nchini Nigeria (MVP) 2023/2024.

“Moja ya sifa kubwa ya Okajepha ni kuhakikisha eneo la ulinzi linakuwa salama muda wote wa mchezo pamoja na kupiga safi na kwenda mbele na kuongeza mashambulizi,” ilifafanua taarifa ya Simba.

“Ubora na umri wake ni miongoni mwa sifa zilizo tuvutia kuhitaji saini yake na tunaamini atakuwa msaada mkubwa kwa timu kuelekea msimu ujao wa Ligi wa 2024/25.” Taarifa ya Simba kuhusu   mchezaji huyo.

Ongezeko la Okejepha linaifanya Simba kuwa na viungo watano wa ulinzi katika kikosi chake msimu ujao, wengine wakiwa ni Mzamiru Yassin,Deborah Fernandes Mavambo, Fabrice Luamba Ngoma na Yusuf Kagoma.

Idadi ya viungo wa ulinzi ambayo Davids amekuwa akipendelea kuipanga katika timu anazofundisha ni wawili katika mfumo wa 4-2-3-1 hivyo viungo hao watano hapana shaka wataingia vitani kuwania nafasi mbili za kucheza katika mchezo mmoja.

Wachezaji hao watano, kila mmoja ana silaha yake ambayo kama akiitumia vyema inaweza kumbeba mbele ya kocha mpya ambaye sura ya kikosi chake cha kwanza itaanza kuonekana katika mashindano ya ngao ya jamii yatakayochezwa mwezi ujao.

Ngoma licha ya kutokuwa mzuri katika ukabaji, amekuwa msaada mkubwa katika kuichezesha Simba pindi inapokuwa na mpira na mchango wake mara nyingi umekuwa ukionekana pale anapocheza na kiungo anayemudu vyema kuilinda safu ya ulinzi.

Mzamiru na Kagoma wana uwezo mkubwa wa kukaba na kupora mipira kutoka kwa timu pinzani pindi zinapojenga mashambulizi lakini wana udhaifu katika upigaji wa pasi sahihi.

Uwezo mkubwa wa kuchezesha timu na kukaba unaonekana unaweza kuwabeba zaidi Mavambo na Okejepha mbele ya kocha Fadru Davids ingawa wote wawili wamekuwa na udhaifu wa kuacha nafasi zao mara kadhaa na kusogea kushambulia jambo ambalo huwa linaacha mianya ambayo inaweza kutumiwa na timu pinzani kutengeneza au kufunga mabao.

Ukiweka kando ushindani huo wa nafasi kwa viungo wa ulinzi, idadi kubwa ya viungo washambuliaji ambao Simba itakuwa nao msimu ujao, inaweza kumpa wakati mgumu kocha Fadru katika utoaji nafasi kwa viungo watatu wa kushambulia kwenye kikosi chake.

Viungo wa pembeni, Simba itakuwa na Ladack Chasambi, Edwin Balua, Kibu Denis, Joshua Mutale na pia Salehe Kalabaka huku pia Valentino Mashaka ambaye amenaswa kutoka Geita Gold pia akimudu kucheza katika nafasi hizo.

Kama kocha Davids ataamua kujikita na mfumo huo mara kwa mara, maana yake ni viungo wawili tu wa pembeni kati ya hao sita ambao watakuwa kikosini huku wengine wakiwa benchi au kutazama mechi jukwaani na kwenye luninga.

Vita nyingine ambayo inaonekana kuwa ngumu ni ile ya kiungo anayecheza nyuma ya mshambuliaji ambayo itawahusisha Jean Charles Ahoua na Awesu Awesu ambao wote wana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho na ubunifu wa kufungua safu za ulinzi za timu pinzani.

Aliyekuwa kaimu kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema kuwa usajili unaofanywa na timu hiyo unazingatia mahitaji ambayo yalijionyesha katika msimu uliomalizika.

Mgunda alisema suala la wachezaji kushindania nafasi ndio kipimo cha ubora wa timu hivyo anaamini msimu ujao unaweza kuwa mzuri kwao.

“Usajili unatokana na tathmini ya msimu uliomalizika ya maeneo gani ambayo yanatakiwa kuimarishwa na yale ambayo yanatakiwa kuzibwa hivyo niupongeze uongozi kwa kufanikisha usajili wa wachezaji wazuri na wenye rekodi nzuri huko walikotoka.

“Baada ya hapo, jukumu linabakia sasa kwa wachezaji kila mmoja kuonyesha kile alichonacho ili benchi la ufundi liweze kumpatia nafasi. Mwalimu ni mpya hivyo kwa sasa wachezaji wote wana nafasi sawa kwa vile hawafahamu hivyo yule ambaye atajituma atajiweka pazuri kwa kocha,” alisema Mgunda

SOMA NA HII  TULIKAA KINYONGE SANA...MUDA WA KUFURAHI NA KUNUNA UMERUDI...LIGI KUU YA MOTO