Home Habari za Yanga Leo GAMONDI ASHITUKIA JAMBO KUBWA YANGA…MECHI ZA CAF

GAMONDI ASHITUKIA JAMBO KUBWA YANGA…MECHI ZA CAF

Habari za Yanga leo

YANGA ina uhakika mkubwa wa kuimaliza mechi ya marudiano dhidi ya Vital’O ya Burundi kwenye Uwanja wa Mkapa Jumamosi baada ya ushindi mabao 4-0 wikiendi iliyopita.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi mwili wake upo Dar es Salaam lakini akili ipo Addis Ababa, Ethiopia kwenye mechi ya marudiano ya CBE ya huko na SC Villa ya Uganda.

Mshindi wa mechi hiyo atacheza na Yanga ambayo inahitaji japo sare yoyote kusonga mbele. Villa ililala mabao 1-2 nyumbani.

Endapo Yanga itafuzu na kukutana na mshindi kati ya CBE au Vila, mabingwa hao wa soka Tanzania wataanzia ugenini kati ya Septemba 13-15 kisha kurudiana hapa nchini kati ya Septemba 20-22.

Gamondi ameangalia rekodi za Yanga dhidi ya timu za Ethiopia akaamua kujiongeza na kutuma watu haraka ambao wikiendi hii watakuwa jukwaani wakiangalia mechi hiyo.

Rekodi zinaonyesha kwamba kwenye michuano ya CAF Yanga haijawahi kushinda nchini Ethiopia.

Kati ya Kocha wao msaidizi Mussa Nd’ew au mtaalam wa kuwasoma wapinzani Msauz Mpho Maruping, mmoja wao ataongoza msafara wa watu wawili kwenye kuisoma CBE ambao taarifa zao za awali imepenyezewa kwamba jamaa wanacheza soka la pasi nyingi na kasi hatua ambayo wanataka kuwajua zaidi haraka kabla ya kukutana nao.

CBE ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchukua ubingwa wa kwao kwa mara ya kwanza tangu ianzishwe 1982.

Timu hiyo imeshiriki mara mbili mashindano ya Afrika ambapo mara mbili ikicheza Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa hatua ya mtoano miaka ya 2005 na 2010 kabla ya msimu huu kuja kutanua historia yao kwa kucheza ligi ya mabingwa.

Kocha wa Yanga Miguel Gamondi ingawa hakutaka sana kuwazungumzia wapinzani hao akidai bado anataka kumalizana kwanza na Vital’O lakini Mwanaaspoti linafahamu ameshawaachia mabosi wake mahitaji ya kutaka kuwajua wapinzani wao.

Mbali na safari hiyo pia Yanga ina mkanda wa video wa mechi ya kwanza kati ya Villa na CBE ambao Waganda hao walijikuta wakikubali kipigo hicho kisha baadaye kucheza pungufu kufuatia mchezaji wao mmoja kupewa kadi nyekundu dakika za mwisho za mchezo.

“Tunataka kuhakikisha kila kitu tunakinasa mapema, hatutaki kuidharau timu yoyote ndio maana unaona tunapambana kuhakikisha tunatuma watu huko Ethiopia na hapa ni safari ya masaa matano tu,”alisema bosi mmoja wa juu wa Yanga.

SOMA NA HII  FEI TOTO:- GSM ANAINGIZA PESA KWA KIPAJI CHANGU...ANADHARAU SANA YULE...