Home Habari za Simba Leo NSIMBA YAWATULIZA MASHABIKI ZAKE…KAULI NI MOJA TU

NSIMBA YAWATULIZA MASHABIKI ZAKE…KAULI NI MOJA TU

HABARI ZA SIMBA

MFUNGAJI wa bao pekee katika mechi ya jana kati ya Simba na Coastal Union, Salehe Karabaka, amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa wasiwe na wasiwasi na timu yao msimu huu kwani itafanya makubwa, akisema ushindi wa bao 1-0 uliopatikana na kushika nafasi ya tatu kwenye Ngao ya Jamii ni mwanzo tu wa shughuli ya msimu mzima.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa kutafuta nafasi tatu ya michuano ya Ngao ya Jamii jana, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Karabaka alisema ametumwa na wachezaji wenzake kuwaambia wanachama na mashabiki wa timu hiyo hawapaswi kuwa na hofu kwani wapo kwa ajili ya kupambana kuipigania nembo ya Simba.

“Kwa niaba ya wachezaji, ni kwamba tumejiandaa vizuri kwa ligi, Jumapili tunaanza kazi, wajitokeze ndiyo kwanza shughuli inaanza, tunataka kila tunapokwenda kucheza wajitokeze kwa wingi uwanjani ili watushangilie,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo, alisema ulikuwa mgumu kwa sababu wapinzani wao nao walijiandaa na walionekana wamepania kucheza hiyo mechi kuliko hata ilivyokuwa dhidi ya Azam FC.

Karabaka pia alisema amefurahi kuweka rekodi ya kucheza mechi ya kwanza msimu huu na kufunga bao kama ilivyokuwa kwenye Kombe la Mapinduzi mwaka jana, alipocheza dhidi ya JKU.

“Mwaka jana Kombe la Mapinduzi nilicheza mechi ya kwanza tu baada ya kusajiliwa na Simba, nikafunga bao dhidi ya timu niliyotoka, JKU na leo nimecheza mechi ya kwanza ya msimu nimefunga bao, tena dhidi ya timu ambayo nimeshawahi kuichezea, Coastal Union, hii ni rekodi yangu nzuri sana kama mchezaji,” alisema Karabaka ambaye alikuwa mwiba kwa mabeki wa timu pinzani jana.

Alifunga bao hilo dakika ya 10 ya mchezo, baada ya kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji kadhaa wa Simba.

Mpira ulianzia kwa beki wa kulia Kelvin Kijili, ambaye alipanda nao kwenye wingi ya kulia, akapiga krosi katikati iliyomkuta Joshua Mutale ambaye naye aliipeleka kwenye wingi ya kushoto alikokuwa Steven Mukwala, kisha akaukokota mpira akiwa pembeni kabla ya kupiga krosi iliyomkuta mfungaji akiwa katikati ya wachezaji wanne wa Coastal Union, akawazidi ujanja na kuuweka wavuni.

Timu zote mbili zililazimika kucheza mechi hiyo ya kusaka mshindi wa tatu baada ya kufungwa mechi zilizopita, Alhamisi, Coastal ikibamizwa mabao 5-2 dhidi ya Azam na Simba ikafungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga.

SOMA NA HII  KUHUSU WACHEZAJI SIMBA KUDAI DAI POSHO ZAO..... UONGOZI WAFUNGUKA HAYA