Home Habari za Simba Leo SIMBA BABA LAO NGAO YA JAMII…REKODI ZAKE WEEE USIPIME

SIMBA BABA LAO NGAO YA JAMII…REKODI ZAKE WEEE USIPIME

habari za SIMBA NA YANGA

Mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na historia na rekodi za timu hizi.

Rekodi zinaonyesha, tangu mwaka 2001 zilipoanza kuchezwa mechi za Ngao ya Jamii, Simba inaongoza kubeba taji hilo mara nyingi , 10, inafuatiwa na Yanga mara saba, kisha Mtibwa Sugar na Azam zilizochukua mara moja, Mbali na hapo, hakuna timu nyingine iliyowahi kushinda Ngao ya Jamii.

REKODI ZA NYUMA TANGU 2001

Mpaka sasa zimechezwa fainali 19 za Ngao ya Jamii kuanzia 2001, huku ikionyesha mwaka 2004, 2006, 2007 na 2008 haikuchezwa, ikaendelea 2009 hadi sasa.

Mara ya kwanza zinaanza kuchezwa mechi hizo, Yanga iliichapa Simba mabao 2-1, wafungaji wa Yanga ni Edibily Lunyamila na Ally Yusuph ‘Tigana’ huku la Simba likifungwa na Steven Mapunda ‘Garincha’.

Mara ya mwisho mwaka jana Simba iliifunga Yanga 3-1 kwa penalti baada ya dakika tisini matokeo kuwa 0-0.

Simba na Yanga katika Ngao ya Jamii zimekutana mara tisa huku rekodi zikionyesha Simba imeshinda mechi tano na Yanga ikishinda nne.

Yanga inakumbuka misimu mitatu nyuma iliifunga Simba mara mbili mfululizo 2021 na 2022 kabla ya Simba kulipa kisasi mwaka 2023.

Mchezo huu wa Simba dhidi ya Yanga utakuwa ni wa nne mfululizo tangu 2021, hivyo ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa ikizingatiwa katika Kipindi hicho Yanga imeshinda mbili na Simba moja, safari hii itataka kushinda ili kuweka mzani sawa kwenye mambo mawili.

Kwanza kubeba taji lao la 11 la Ngao ya Jamii na kuikimbia zaidi Yanga, kisha kushinda ili nayo iwe imeshinda mara mbili katika nne walizokutana hivi karibuni ndani ya michuano hiyo.

Yanga yenyewe inataka kuendeleza ubabe mbele ya Simba kwani tangu mara ya mwisho ipoteze katika Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao hao, wakaja kushinda mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara 2023-2024 tena kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-2. Ile ya kwanza ilikuwa Simba 1-5 Yanga kisha Yanga 2-1 Simba.

 

USHINDANI SASA

Ukiangalia vikosi vya timu zote mbili vina mabadiliko ya wachezaji, lakini Simba ndiyo ina maingizo mapya mengi ambayo yamefika 14, wakati Yanga wachezaji wapya ni saba.

Majembe mapya ya Simba yanayotarajiwa kuibeba timu hiyo ni raia wa kigeni wanane ambao ni Valentin Nouma, Chamou Karabou, Charles Ahoua, Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Joshua Mutale, Steven Mukwala na Moussa Camara.

Wazawa ni Kelvin Kijiri, Abdulrazack Hamza, Yusuph Kagoma, Awesu Awesu, Omary Omary na Valentino Mashaka. Lameck Lawi alikuwa wa kwanza kutambulishwa lakini usajili wake umezua utata, hata hivyo hayupo kambini na ametimkia Ulaya.

Wachezaji saba wapya wa Yanga ni Khomeny Abubakari, Chedrack Boka, Clatous Chama, Aziz Andabwile, Duke Abuya, Prince Dube na Jean Baleke. Wazawa wawili pekee kwenye listi hiyo Khomeny na Andabwile.

Usajili wa pande mbili kwa timu hizo ndiyo unaufanya mchezo huu kusubiriwa kwa hamu kwani Simba inaamini imeimarisha kikosi chao wakati Yanga ikitamba imefanya maboresho kidogo tu yanayoweza kuwapa tena furaha.

Simba na Yanga mwaka huu kwao itakuwa ni mara ya 15 kushiriki Ngao ya Jamii. Simba ikiwa imeshinda Ngao ya Jamii 10, imepoteza nne, wakati Yanga imeshinda saba na kupoteza saba.

Mchezo huu utatoa picha ya hali halisi ya timu hizi na jinsi zinavyokabiliana na changamoto za msimu mpya.

SOMA NA HII  DILI LA OPUKU KUTUA SIMBA SC LAFIA KWENYE MAKARATASI...ISHU NZIMA IKO HIVI....