Home Habari za Simba Leo SIMBA, YANGA ZAWEKEANA MTEGO MECHI YA KESHO

SIMBA, YANGA ZAWEKEANA MTEGO MECHI YA KESHO

Habari za Yanga Leo

KESHO KITAELEWEKA, Ni Simba na Yanga fainali ya Ngao ya Jamii katika dimba la Mkapa kitawaka. Simba amesajili wachezaji kibao akiwemo Debora Fernandez Mavambo, Okejepha na Ahoua, huku Yanga akiwa na Jeshi lake kamili likiwa na nguvu ya Prince Dube, Baleke na Chama.

Timu zote mbili zimecheza michezo kadhaa ya kirafiki ikiwemo katika matamasha yao ya Wiki ya Wananchi, na Simba Day, ambapo wote waliweza kushinda mechi hizo. Lakini kila timu imeweka mtego wake kuelekea mechi ya kesho.

MTEGO WA SIMBA

Katika michezo minne ambayo Simba imecheza ya kirafiki tangu ilipoweka kambi ya wiki tatu huko Ismailia, Misri dhidi ya Al-Adalah (2-1), Telecom FC (2-1) na El Qanah FC (3-0) na mmoja wa Simba Day dhidi ya APR (2-1) imefunga jumla ya mabao tisa, mawili yamefungwa na Jean Charles Ahoua huku Augustine Okejepha, Valentino Mashaka, Ladack Chasambi, Steven Mukwala, Joshua Mutale, Edwin Balua na Fernandes wakifunga moja kila mmoja.

Katika michezo hiyo, Fadlu alikuwa akifanya machaguo tofauti ili kupata kikosi chake cha maangamizi jambo ambalo limemfanya kuwa na wachezaji tofauti hasa katika maeneo ya ushambuliaji wenye uwezo wa kutengeneza nafasi na kufunga.

Ubora ambao Simba wameonyesha eneo la ushambuliaji, kuanzia eneo la kiungo mchezeshaji hadi pembeni kwa mawinga ni wazi kwamba kutakuwa na vita dhidi ya ukuta wa Yanga ambao umeboreshwa kwa kusajiliwa kwa Chadrack Boka upande wa beki ya kushoto.

Katika namna ambavyo Fadlu ameonekana kukisuka kikosi chake kuwa na staili tofauti za kushambulia, mfano mzuri ni namna walivyocheza katika mchezo wa Simba Day dhidi ya APR, ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, Mutale na Awesu walikuwa wakiongeza idadi ya viungo washambuliaji, walisogea eneo la wapinzani kwa kuingia ndani, Shomary Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndio waliokuwa huru kushambulia maeneo ya pembeni.

Ukuta wa Yanga ambao unaongozwa na kipa, Djigui Diarra umeruhusu mabao matatu katika michezo minne iliyocheza ya kirafiki mawili dhidi ya FC Augsburg ya Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ na moja dhidi ya Red Arrows F.C.

Udhaifu ambao Yanga imeonakana kuwa nao katika ukuta wake, ni kuruhusu bao la kichwa dhidi ya Red Arrows huo ni ugonjwa ambao wamekuwa nao tangu msimu uliopita, huku mabao dhidi ya Augsburg ikiwa ni uzembe wa kushindwa kwa mabeki wake kukaa katika maeneo sahihi kiasi cha kuacha mianya wazi.

ni dhahiri kuwa eneo la Simba la ushambuliaji litakuwa na mawinga, Joshua Mutale, Awesu Awesu, viungo wa kati,Debora Fernandes,Jean Charles Ahoua na huku Steve Mukwala akisimama kama mshambuliaji wa mwisho.

MOTO WA YANGA

Hii ni vita nyingine kali kati ya safu ya ushambuliaji ya Yanga yenye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, Stephane Aziz Ki dhidi ya ukuta wa Simba wenye maboresho mawili yaliyofanywa katika dirisha hili la usajili, kipa kutoka Horoya ya Guinea, Moussa Camara na beki wa kati, Chamou Karaboue.

Ni wazi kuwa ukuta wa Simba ambao umeruhusu mabao mawili katika michezo yake ya kirafiki utakuwa na kazi kubwa ya kufanya kutokana na Yanga kuimarisha eneo lake la ushambuliaji kwa kuwaongeza kundini, Duke Abuya, Prince Dube, Jean Baleke na Clatous Chama ambaye anajitafuta.

Abuya na Dube wanaonekana tayari kuwaka na wanaweza kuiweka Simba katika wakati mgumu kutokana na kile walichokifanya katika michezo ya kirafiki kwa kushirikiana na Aziz Ki, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua na Clement Mzize.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga ilishtua Afrika Kusini kwa kuitandika Kaizer Chiefs mabao 4-0 kwenye michuano ya Toyota, Aziz KI alifunga mara mbili, Dube na Mzize kila mmoja alicheka na nyavu.

Namna ambavyo Yanga imekuwa ikisaka matokeo imekuwa haitabiriki, inaweza kushambulia kupitia maeneo yake ya pembeni (winga ya kushoto na kulia) na hata kati ambako amekuwa akicheza Aziz Ki na wakati mwingine Mudathir Yahya.

Hivyo inaonekana safu yake ya ushambuliaji kesho itakuwa na mawinga, Max Nzengeli,Prince Dube, viungo wa kati, Duke Abuya, Aziz KI huku mshambuliaji wa kati akiwa Clement Mzize.

SOMA NA HII  MTU WA KUCHUNGWA ZAIDI AL AHLI VS SIMBA.