Home Uncategorized FOWADI MPYA YANGA USIPIME

FOWADI MPYA YANGA USIPIME


HUYO Makambo wenu mtamsahau! Ndivyo unaweza kusema kufuatia fowadi mpya ya Yanga kuonekana ni moto na hii ni kutokana na takwimu zake za kutupia mabao.

Yanga msimu uliopita ilimtegemea zaidi Heritier Makambo raia wa DR Congo ambaye akiwa Jangwani aliwajaza wapinzani kwa kufunga mabao 17 kwenye ligi kuu na sasa amewapa mkono wa kwaheri kuelekea Horoya AC ya Guinea.

Baada ya kubaini hilo, Yanga chini ya uongozi mpya ukiongozwa na mwenyekiti msomi, Mshindo Msolla umefanya usajili wa fasta sana ili kuhakikisha unawasaini wachezaji ambao Kocha Mwinyi Zahera amewahitaji tayari kwa kwenda nao kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Agosti mwaka huu.

Mpaka sasa Yanga imenasa saini za washambuliaji watatu wa kimataifa ambao ni Mnamibia, Sadney Urikhob, Mrundi, Issa Bigirimana ‘Walcott’ kutoka APR ya Rwanda na Maybin Kalengo (Zesco, Zambia) hawa wote unaambiwa ni tishio kwelikweli.

Wachezaji wengine waliosaini Yanga ni, kipa wa Bandari FC ya Kenya, Farouk Shikalo Erick Rutanga kutoka Rayon Sports ya Rwanda, Lamine Moro (Buildcon, Zambia), Abdul Aziz Makame (Mafunzo FC, Zanzibar) na Ally Mtoni Sonso (Lipuli FC, Iringa). Yanga imeachana na Makambo na tegemeo ni kwa Urikhob ambaye alisaini mkataba wa miaka mitatu na kurejea kwao fasta ikiamini kuwa atafanya mambo makubwa zaidi ya Mkongomani huyo.

Championi limeangalia takwimu za Urikhob na kubaini kuwa amekuwa na wastani mzuri wa kufumania nyavu ambayo haina tofauti sana na aliyoiweka Amissi Tambwe tangu alipotua nchini na kucheza Simba kisha baadaye Yanga.

Tambwe anashikiria rekodi ya kufunga mabao 90 katika mechi zaidi ya 120 alizocheza katika mashindano mbalimbali akiwa na Simba na Yanga kuanzia msimu wa 2013/14 ambapo alitua hapa nchini akitokea Vital’O ya Burundi.

Urikhob yeye anashikilia rekodi ya kufunga jumla ya mabao 64 katika klabu mbambali alizozitumikia kuanzia msimu huo mpaka hivi karibuni alipoamua kujiunga na Yanga. Rekodi ambazo Championi Jumamosi limezipata kuhusiana na Urikhob zinaonyesha msimu 2013/14 akiwa na timu ya AmaZulu inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini alifunga mabao tisa katika mechi 20 alizocheza.

Msimu wa 2014/15 akiwa na kikosi cha Saraburi cha nchini Thailand aliifungia mabao 12 katika michezo 30. Kasi yake ya utupiaji mabao ilizidi kuongezeka kwani msimu wa 2016/17 akiwa na kikosi cha Super Power Samut Prakan ya nchini Thailand alitupia mabao 15 katika mechi 42.

Ukichana na timu hiyo, mwaka 2017 akiwa na kikosi cha timu BEC Tero Sasana ambayo pia inashiriki Ligi Kuu ya Thailand alifunga mabao sita tu katika mechi 17, huku mwaka uliofuata akiwa na kikosi cha PSMS Medan ya Indonesia alifunga mabao tisa katika mechi 11.

Timu yake ya mwisho kabla ya kutua Yanga ni Tura Magic ya Namibia ambayo ameitumika mechi 15 na amefunga mabao 13 hii inaonyesha kuwa mshambuliaji huyu tayari ana uzoefu na ligi tafu hasa kwa kuangalia klabu alizopita tofauti na kwa Makambo
ambaye alicheza DC Motema Pembe na FC Saint Eloi za DR Congo.

Kwa takwimu hizi ni wazi kuwa Yanga imelamba dume kama itampa muda zaidi wa kuzoea soka la Bongo ambalo wapinzani huwa hawapendi kuona mchezaji wa timu pinzani akifanya vyema. Aidha rekodi za Bigirimana zinaonyesha kuwa amekuwa mwepesi zaidi wa kuwatengenezea wenzake nafasi za mwisho ndiyo maana amefunga mabao sita tu katika michezo 21 aliyocheza kwenye ligi.

Hata hivyo kuhusiana na usajili wa Urikhob na mastaa wengine kikosini hapo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela aliliambia Championi Jumamosi kuwa, kabla ya kupewa nafasi na Caf ya kushiriki michuano hiyo kimataifa usajili wao mpya ulilenga kusuka kikosi imara watakachokitumia kwa ajili ya michuano yote ya msimu ujao.

Mwakalebela alisema, nafasi waliyoipata ya kushiriki michuano hiyo mikubwa Afrika imekwenda sawa na malengo yao kutokana na aina ya wachezaji ambao wamewasajili hadi hivi sasa.

“Mipango yetu kukiimarisha kikosi chetu kwa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu watakaotoa ushindani, kama mnavyoona usajili wetu huo tunaoendelea kuufanya wa wachezaji,” alisema Mwakalebel

SOMA NA HII  KMC WALITAKA TAJI LA KOMBE LA SHIRIKISHO