Home Uncategorized KESI YA MALINZI NGOMA BADO MBICHI, UAMUZI WA KESI SASA JULAI 23

KESI YA MALINZI NGOMA BADO MBICHI, UAMUZI WA KESI SASA JULAI 23


Hatimaye kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Jamal Malinzi na wenzake upande wa Serikali  umefunga ushahidi rasmi na  mahakama inatarajiwa  kutoa uamuzi  Julai 23, mwaka huu  ili kufahamu kama wanakesi ya kujibu au laa.

Malinzi anashatikiwa na wenzake ambao ni Celestine Mwesigwa aliyekuwa katibu wa TFF, Nsiande Mwanga (Mhasibu), Mariamu Zayumba (Meneja Ofisi TFF) na Frola Rauya (karani) na hawa wote walikuwa wanafanya kazi TFF.


Wakili wa Serikali, Leonard Swai aliiambia mahakama kuwa, wamefunga rasmi ushahidi wao baada ya kupeleka mashahidi 15 na kutoa ushahidi kuhusiana na kesi hiyo.

Lakini kabla ya kufunga ushahidi huo, Swai aliiomba mahakama kufanyia marekebisho baadhi ya mashitaka ambayo yaliainishwa katika hati ya mashitaka.

Swai aliiomba mahakama kufanya marekebisho hayo chini ya kifungu 234 ambapo wamefanyia marekebisho katika  mashitaka matano kati ya yale 28 ambayo yaliainishwa katika hati ya mashitaka.

Mashitaka yaliyofanyiwa marekebisho ni pamoja na shitaka la pili ambalo linamhusu  Malinzi na Mwesigwa lile la matumizi mabaya ya madaraka.

Shitaka la tatu la kughushi nyaraka ambalo linawahusu wote wawili tena na shitaka la nne la Celestine Mwesigwa la kuwasilisha nyaraka za uongo, shitaka la 18, 19 yanamhusu Malinzi pekee ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, akidai aliikopesha TFF.

Baada ya kufanyiwa marekebisho mashitaka  hayo, washitakiwa walisomewa upya mashitaka hayo na yote waliyakana.


Hakimu Mkazi Mwandamizi, Maira Kasonde wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alisema washitakiwa wana haki ya kuomba  mashahidi waliotoa ushahidi kuomba waulize maswali au kutoa ushahidi upya lakini washitakiwa walikubali kuendelea na kesi bila mashahidi kuitwa upya.

Kasonde alisema ushahidi umefungwa kwa upande wa Serikali na kesi ijayo itatolewa uamuzi ambapo tukio hilo litakuwa Julai 23, mwaka huu. 

SOMA NA HII  TAIFA STARS KAMILI KUIVAA BURUNDI, KUINGIA KAMBINI LEO