Home Uncategorized MAHAYAWANI WA AFRIKA KUSINI WANAVYOZIDIWA UFIKIRI HATA NA MPIRA UNAOCHEZWA UWANJANI

MAHAYAWANI WA AFRIKA KUSINI WANAVYOZIDIWA UFIKIRI HATA NA MPIRA UNAOCHEZWA UWANJANI





Na Saleh Ally
 UTAKUWA unajua mengi sana kuhusiana na mchezo wa soka lakini huenda kwa nguvu yake unaweza usiwe na kipimo sahihi!


Nakuuliza kwanza hivi nani aliyekuwa na akili ya kuanzisha kale “kamduara” ambako leo kanaendesha dunia? Maana kila unavyojaribu kufuatilia, si Waingereza, Wachina na Waafrika, kila upande unavutia kwake, kwamba ndiyo chanzo.
Hakuna anayekubali kuachwa nyuma kuhusiana na mpira ambao uko katika aina mbalimbali na unatumika katika michezo mbalimbali duniani.

Inawezekana ukubwa wa mpira unafanya kila upande usikubali kuonekana hauhusiki au sio chanzo na ukubwa wake si viwanjani tu, badala yake katika maeneo mengi makubwa.

Mfano mzuri angalia hapa nyumbani Tanzania namna ambavyo wanasiasa wamekuwa wakilazimika kurejea katika mpira kupata kile ambacho wanataka.

Kawaida wanasiasa wanapenda kule ambako kuna mkusanyiko wa watu. Mpira ambao ni kitu kidogo sana kwa mwonekano, hakina shepu yenye mvuto hivyo lakini nguvu yake ni kubwa sana.

Watu wengi wangependa kwenda uwanjani kushuhudia mpira ukichezwa. Hapa anayechezwa ndiye anayewakusanya watu kwa maana kwamba wacheze lakini watazamaji nao wanataka kuuona ukichezwa na mwisho linakuwa suala la burudani na biashara kwa kuwa mpira pia ni tegemeo kubwa la maisha ya watu.

Wakati wengine wanaburudika, wako wanaishi kupitia mpira huo ukianzia wachezaji, viongozi, wanahabari na kadhalika. Mpira ni mkubwa sana na inawezekana una “akili” nyingi sana.



Kilichonifanya nianze kutafakari na kukumbuka kuhusiana na mpira ni kuhusiana na lile suala la ubaguzi wa rangi wa Waafrika wenyewe kwa wenyewe, jambo la kipuuzi ambalo Afrika imelishuhudia kwa muda mwingi sasa.

Nimeshuhudia baadhi ya video ambazo hakika hazitazamiki, zinaumiza moyo na kuacha alama ya makovu ndani ya moyo. Namna ambavyo Waafrika wanavyowachoma moto Waafrika wenzao ambao hawana hatia, hawajawaibia wala kuwadhulumu.

Wanawaua kinyama kwa kuwa Waafrika hao wamewazidi uwezo wa kujituma na kujiingizia kipato. Vijana wengi wa Afrika Kusini ni wenye midomo mingi, si watu wanaojituma na pombe na “mademu” ndio kinachowavutia.

Juhudi za wale wanaochapa kazi, zinawafanya wafanikiwe kwa kuwa tundu la wengi kukimbilia nchini humo ni kutokana na kuwa na fursa za kibiashara wakati wenyeji wakiwa hawazichangamkii.

Umeona, nchi mbalimbali kama Nigeria na nyingine wameanza kuchukua hatua za kuwashambulia. Huenda si nzuri lakini wamechoshwa. Unaona Zambia wamelazimika kuahirisha mechi yao ya kirafiki dhidi ya Afrika Kusini maana waliona isingekuwa kuna uhakika wa usalama kwa kuwa wachezaji wa Bafanabafana wangeweza kushambuliwa.

Ni jambo ambalo limenikera sana na kushangazwa na Serikali ya Afrika Kusini kutolivalia njuga. Wakati natafakari hilo, nikaanza kuwaza namna ambavyo mpira mdogo unavyoweza kuunganisha watu kwa kiwango cha juu kabisa.

Mpira wa soka unaweza kuwaunganisha waliogombana kikabila au kidini na umetumika katika nchi nyingi kulipokuwa na matatizo. Mfano mzuri ni nchi jirani ya Rwanda ambao mwaka 1994 kulikuwa na mauaji ya kimbari.

Wakati wameanza kuondoka kwenye vita, kilichofanyika ni kuutumia mpira kuwaunganisha Watutsi na Wahutu ambao wasingeweza kukaa pamoja.

Lakini kwa kuwa katika mpira, katika ushangiliaji mfano timu za APR na Rayon Sports, unakuta Mhutu na Mtutsi wanashangilia timu moja au Mhutu na Mhutu timu tofauti.

Hii ikaongeza nguvu ya kuwasahaulisha watu wa makabila haya mawili na kuwaunganisha kuwa wao ni kitu kimoja. Hii imetumika karibu katika nchi zote za Ulaya, Afrika, Uarabuni na kwingineko ambazo zilikumbwa na vita.

Wakati wa kurekebisha hali ikae sawa, mpira ndio ukatumika kuwasogeza watu karibu na inaonekana katika nchi zilizokuwa na vita kwa 58%, mpira umetumika kama kiunganishi cha kusahau machungu au makovu ya vita na mafanikio yamekuwa kwa 76%.

Mpira ndio unaonekana una mafanikio makubwa zaidi katika kuwaunganisha waliotoka katika machungu ya vita ambayo hujengwa na maumivu makali kwa kuwa kunakuwa na mauaji, watu wamepoteza nguvu, watoto au wazazi na kazi ya kuwasahaulisha hilo, si jambo dogo.

Sasa najiuliza, kama mpira tu ambao hata Afrika Kusini upo unawaunganisha watu kwa kiwango cha juu. Vipi hawa watu wenye akili zao timamu, waliotoka kulalamika kuwa walibaguliwa leo wanaamua kujibagua wao wenyewe!

Maana wanawabagua watu wenye rangi na nywele kama zao. Wakati wakibaguliwa walilia kuwa Wazungu warudi kwao, Afrika ni ya Waafrika lakini leo wanasema Waafrika wengine warudi kwao na Afrika Kusini si kwao wakiwa wamesahau wazazi wao walikaa katika nchi wanazotokea wanaowaua na kuwadhulumu hii leo.

Mpira kweli una akili na tunapaswa kuthamini sana. Nguvu yake tunapaswa kuiona, kuijali na kuithamini kwa kuwa ina faida kubwa kuliko rundo la watu kutoka Afrika Kusini.
SOMA NA HII  KAGERE AMALIZA SHUGHULI TAIFA, AACHA KILIO KWA NAMUNGO KWA BAO LAKE LA USIKU