Home Uncategorized NAMNA TAMBWE ANAVYOTUONYESHA MAKOSA YA USAJILI KATIKA KLABU ZETU

NAMNA TAMBWE ANAVYOTUONYESHA MAKOSA YA USAJILI KATIKA KLABU ZETU




NA SALEH ALLY
SASA Yanga tayari imecheza mechi 27 za Ligi Kuu Bara na mchezaji anayeongoza kwa mabao ya kufunga katika kikosi hicho ana nane.

David Molinga raia wa wa DR Congo ambaye alisajiliwa wakati msimu unaanza Yanga ikiwa chini ya Mkongoman, Mwinyi Zahera amefunga mabao hayo nane na bila ubishi, hayatoshi kwa kuwa ya mfungaji tegemeo wa kikosi.

Inawezekana ikawa hivyo kama Yanga ingekuwa na wigo mpana wa wafungaji wa mabao kwa maana kuwa na viungo wanaofunga mabao mengi. Lakini kama ni timu yenye mshambuliaji hatari na inamtegemea, basi lazima awe na mabao mengi hasa na mfano mzuri ni Meddie Kagere ambaye pamoja na watu kumdhihaki, sasa anaongoza akiwa na mabao 19, maana yake, mara mbili zaidi ya Molinga.

Ukiangalia Yanga ina mabao 31 ya kufunga katika mechi 27, jambo ambalo linadhihirisha kuwa tatizo kubwa kabisa la Yanga msimu wa 2019/20 ni mabao ya kufunga.

Unaona wakati Yanga ina 31 katika mechi 27, watani wao Simba baada ya mechi 28, wamefunga mabao 63.

Kwa wingi wa mabao ya kufunga, Yanga inashika nafasi ya tano baada ya Simba, Azam FC wenye 37, Kagera Sugar wenye 36 na Namungo FC 34. Hapa pia ni sehemu ya kujiuliza kuwa vipi timu kama Yanga inaweza kusema inawania ubingwa kwa mwendo wa wafungaji wanaozidiwa hata na wale wa Kagera au Namungo FC, vipi wataweza kukusanya pointi nyingi na idadi kubwa ya mabao?

Makosa makubwa yaliyofanyika katika usajili wa kisiasa mara mbili ndani ya msimu mmoja, inaonyesha wazi kuwa kuna kasoro.

Mfano wakati Yanga waliamua kuachana na wachezaji kadhaa waliokuwa tegemeo kwao na kusajili wapya walisema wanaboresha kikosi lakini haikuwa hivyo.

Kuondoka kwa rafiki wa nyavu, Amissi Tambwe ambaye ilielezwa ‘ameisha’ lakini waliosajiliwa baada ya yeye wakaonekana hawakuwa wamemfikia hata robo.

Angalia Yanga imesajili zaidi ya washambulizi wanne katika msimu mmoja na idadi yao ya mabao haijafikia hata nusu ya mambo aliyofunga Tambwe kwa msimu mmoja.

Tambwe ameondoka Yanga akiwa na rekodi ya aina yake ambayo haitafikiwa na Juma Balinya, Yikpe Gnamien, Molinga na wengine ambao Yanga iliwategemea kwa ajili ya kufunga mabao.

Msimu wa 2013/14 aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 19 akifuatiwa na Kipre Tcheche wa Azam FC aliyekuwa na mabao 13. Msimu uliofuata alijiunga na Yanga akitokea Simba ambako alikuwa amefunga bao moja, akiwa Yanga akafunga mabao 13 na kuwa na 14 akashika nafasi ya pili nyuma ya Saimon Msuva aliyefunga mabao 17.

Msimu wa 2015/16, Tambwe alionyesha si mtu wa kubahatisha kwa kufunga mabao 21 na kuwa mfungaji bora akifuatiwa na Hamisi wa Simba aliyekuwa na mabao 19 na msimu wa 2016/17 akapachika mabao 11 wafungaji bora wakiwa wawili, Msuva na Abdulrahman Mussa, kila mmoja akiwa na mabao 14.

Unaona msimu wa 2017/18, Tambwe haukuwa vizuri baada ya kuandamwa na majeraha, akakaa benchi muda mwingi na Emmanuel Okwi akaibuka akiwa mfungaji bora. Msimu wake wa mwisho wa 2018/19 wakati Kagere anaibuka mfungaji bora kwa kupachika mabao 23 akivunja rekodi yake ya mabao 21, yeye Tambwe alifunga mabao nane na kushika nafasi ya 10 katika msimamo wa wafungaji bora.

Huenda Yanga walikuwa sahihi kusema alikuwa kiwango kimeshuka, huenda walihofia majeraha ya kila mara. Lakini angalia waliokuja kuchukua nafasi yake, mwenye nafuu ni Molinga ambaye angalau ana mabao nane kama ambayo Tambwe aliaga nayo Yanga.

Hili linaweza kuwa fundisho, kwamba wakati wa usajili lazima kile ambacho unakiacha ukitaka kujiimarisha jiridhishe kitakuwa bora kuliko ulichokuwa nacho. Kusajili mchezaji akawa na kiwango cha chini kuliko yule uliyemuacha, maana yake hauko makini.

Mfano mwingine, Paul Nonga aliyekuwa Yanga, sasa ana mabao 11 katika msimamo wa wafungaji sawa na mshambulizi mwingine wa zamani wa Yanga, Reliants Lusajo ambao pia walionekana hawafai Yanga huku wanaofaa wakiwa wanaonekana wana uwezo mdogo na mamilioni yametumika kuwasajili.

Yanga imepata hasara ya mamilioni kwa kusajili wachezaji wasio na msaada na ikalazimika kutumia fedha kwa baadhi yao kuvunja tena mikataba. Ajabu katika dirisha dogo, usajili ukawa hauna tofauti kutokana na rundo la makosa.

Makosa yanaweza yakawa ya kibinadamu yanayoonyesha umakini mdogo au duni. Lakini makosa hayo ya kibinadamu yanaweza yakawa ya makusudi kwa kuwa tu wanaofanya usajili wanakuwa wanafaidika kwa kupata kitu fulani na wanajua klabu haitakuwa na manufaa ili mradi mifuko yao ina kitu, basi ni faraja kwao na hili lazima libadilike na Tambwe atakuwa mfano sahihi wa kujifunza unapofikia wakati wa usajili.

Yanga watumie wataalamu, kama ni kamati iwepo inayojumuisha wataalamu ambao watakuwa wanashirikiana na benchi la ufundi kuleta wachezaji sahihi ambao hata kama ni gharama basi wana uhakika wa kufanya vizuri.

Mfano mzuri ni Bernard Morrison licha ya kwamba aliyeshiriki kumsajili injia Hersi Said si kocha, lakini alifanya kazi nzuri na unaweza kuwa mwongozo mzuri.

Pamoja na hivyo, Yanga lazima wahakikishe katika usajili hasa muda unapowadia suala la wapiga dili lisipewe nafasi maana wanajali kufaidisha matumbo yao na inakuwa tena si kwa faida ya Yanga.


SOMA NA HII  HII HAPA RATIBA YA LIGI KUU BARA KWA MSIMU WA 2019/20 - VIDEO