Home Uncategorized TUJIFUNZE NAMNA MADINI YA AJIBU YALIVYOMALIZIKIA BENCHI…

TUJIFUNZE NAMNA MADINI YA AJIBU YALIVYOMALIZIKIA BENCHI…

Na Saleh Ally
HAKUNA anayelalamika kuhusiana na kiwango cha mshambuliaji Ibrahim Ajibu Migomba kupitia kipaji, badala yake ni neno moja na tunapaswa kujifunza kupitia kwake.

Inawezekana watakaotakiwa kujifunza zaidi ni wale wanaochipukia, wale wanaomuamini na ikiwezekana wale wanaotamani kuwa kama yeye.

Kwa wale ambao wanapenda kuendelea na kufikia matamanio yao kisoka, pia wanaweza kumtumia Ajibu kama somo kuu la kubadili maisha yao kwa kuwa kwa miaka michache tokea ameanza kuwa maarufu, ana kitabu chenye kurasa nyingi za mafunzo.
Kocha Mkuu wa Simba, Sven van derbroeck raia wa Ubelgiji aliamua kumrudisha Ajibu katika kikosi chake cha pili ili apate nafasi ya kutosha ya kucheza na kuwa fiti hasa.

Sven ambaye ni kati ya makocha vijana waliowahi kuinoa Simba, amesema anaamini Ajibu ana kipaji na uwezo wake ni mzuri lakini anamtaka awe fiti ili kuendana na kasi ya kikosi chake.

Pamoja na hivyo, Sven amemsisitiza Ajibu kujituma zaidi ili kuweza kuingia katika kikosi cha kwanza. Hii si mara ya kwanza kwa Ajibu kuambiwa suala “kujituma” kwanza.

Inawezekana wamepita makocha wengi walisema hivyo lakini kama unakumbuka wakati akitokea Simba kwenda Yanga, gumzo kutoka Msimbazi lilikuwa kuwa Ajibu ana kipaji lakini mvivu wa mazoezi na hapendi kujituma.

Baada ya kutua Yanga pamoja na kwamba usajili wake ulikuwa gumzo, kilichotokea ni Kocha Mkuu, George Lwandamina wakati huo aliamua kumuweka benchi na kumpa mazoezi ya ziada.

Lwandamina maarufu kama Chicken aliamini Ajibu ana “madini” lakini utimamu wa mwili ambao hutokana na mazoezi magumu au makali na hasa mwanzoni mwa msimu, haukuwa sawa.

Baada ya mazoezi ya muda mrefu, alianza kumtumia. Hali kadhalika, alipoingia Mkongomani, Mwinyi Zahera naye akaona bado Ajibu alikuwa na upungufu wa utimamu wa mwili kwa maana ya fitness.
Kawaida utimamu wa mwili hulindwa, baada ya kuwa fiti kuna miiko yake ikiwemo kupumzika, kutofanya ngono zembe na kadhalika. Lakini kuendelea kuongeza mazoezi kulinda ulichonacho mwilini.

Unaona alipoingia Zahera naye aliona Ajibu ana kitu ambacho kitakuwa msaada katika kikosi chake lakini mwisho bado akaona upungufu uleule wa utimamu wa mwili.

Alichofanya ni kumuweka katika mazoezi maalum wakiwa kambini ili kuhakikisha anakuwa fiti. Wakati watu wakilalamika, Zahera hakujali akampa Ajibu mazoezi ya kutosha na alipopata nafasi katika kikosi cha kwanza akatumia ujanja kumtaka ajione ana mzigo wa kuibeba timu.

Akamvua unahodha Kelvin Yondani na kumpa Ajibu akiwa nahodha kwa mara ya kwanza katika klabu kubwa kama hiyo. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha anakuwa kiongozi.

Kama unakumbuka hili nalo lilienda kwa muda tu baada ya hapo Ajibu akaanza kukaa benchi akiwa nahodha, hali inayoonyesha alishindwa tena kutunza kiwango chake katika kiwango kinachotakiwa licha ya kwamba alikuwa ni nahodha.

Kila kocha ambaye amemfundisha Ajibu anaona jambo moja na Ajibu ameshindwa kulitatua na hili linamfanya aendelee kubaki benchi wakati akiwa na madini yake.

Kwa kifupi, madini aliyo nayo hayamsaidii Ajibu kwa kuwa anashindwa kuhakikisha anayafanyia usafi. Kuyafanyia usafi ni “simpe” tu, kufanya mazoezi ya uhakika na kuendelea kuyalinda ili aendelee kuwa fiti.

Uvivu ni adui wa maendeleo, kwa wale ambao wamekuwa wakisema ni mvivu basi inawezekana ameshindwa kumshinda adui huyo na ndio maana mwanzo nikasema wanaotaka kuwa kama Ajibu au wanaotaka kutimiza ndoto zao, wamtumie Ajibu kujifunza namna ya kupambana na adui uvivu.

Haiwezekani kasoro moja ikakushinda, ikakunyima nafasi, ikakufanya uonekane hauwezi lakini ukashindwa kupambana nayo wakati ipo ndani ya uwezo wake.

Haiwezekani una neema ya kipaji, ukakosa moyo tu wa kujituma. Ajibu si wa kukaa benchi timu yoyote hapa Tanzania na inawezekana hata angekwenda TP Mazembe alikuwa na nafasi ya uhakika ya kucheza lakini aliamua kutokwenda, huenda kwa kuwa anajitambua.

Kila mtu ana uamuzi wa maisha yake, Ajibu amechagua alivyokuwa zamani na alivyo sasa. Kitu kizuri, mtumieni kwa faida yenu na taifa kisoka, mjifunze badala ya kumshangaa, maana haiwezekani kila kocha mpya, azungumze lilelile kama la kocha aliyepita na bado ushindwe kulibadilisha. 

SOMA NA HII  WAKATI MAMBO MENGINE YAKIENDELEA HUKO SIMBA, KIKOSI KIMESHUKA KAMBINI LEO KWAAJILI HII