Home Uncategorized SUALA LA VIWANJA KUWA BORA LIZINGATIWE ILI KULETA USHINDANI

SUALA LA VIWANJA KUWA BORA LIZINGATIWE ILI KULETA USHINDANI

 


LIGI Kuu Tanzania Bara kwa sasa imeshaanza kutimua vumbi ambapo Septemba 14 ulichezwa mchezo mmoja kati ya Namungo FC na Polisi Tanzania wa kukamilisha mzunguko wa pili.

Tumeona kwamba kila timu inapambana kupata matokeo na kinachopatikana kinaonekana baada ya dakika 90 kukamilika baada ya ligi kuanza kutimua vumbi Septemba 6.

Ushindani umekuwa mkubwa na hali hii inatakiwa kuwa endelevu mpaka mwisho wa msimu ili kufanya kila mchezaji aone thamani ya kushiriki ligi na kucheza kwa kujituma.

Kwa wachezaji nao wana kazi ya kuonyesha kile ambacho wanacho kwenye miguu yao kwa kucheza kwa akili pamoja na nidhamu ili kutimiza malengo yao pamoja na ya timu kiujumla.

Sio kazi rahisi kufikia malengo ikiwa wachezaji watashindwa kutimiza majukumu yao kwa umakini wakishirikiana na benchi la ufundi bila kuwasahau viongozi.

Ipo wazi kwamba mwanzo kila timu huwa inakuwa na shauku ya kuonyesha kile ilicho nacho. Kwa kufanya hivyo kunaongeza ushindani na nguvu ya kila mchezaji kusaka ushindi ndani ya uwanja.

Baada ya usajili kufungwa maana yake kinachotakiwa kufanyika ni kazi ndani ya uwanja na kuacha zile porojo za wakati ule wa usajili.

Nina amini kwamba kila timu imeweka mpango kazi kwa ajili ya kufikia malengo yake. Ili kufikia malengo ni lazima kila mmoja akawa ndani ya timu jambo hili litasaidia kufanikisha mipango kwa wakati.

Tukiachana na hayo sasa hebu tutazame sehemu muhimu ambayo inahusika kutoa ushindi kwa wachezaji wawapo kazini kusaka pointi tatu ambapo ni ndani ya uwanja.

Ubora wa uwanja hasa sehemu ya kuchezea ni muhimu kuwa bora wakati wote ili kutoa burudani kwa wale ambao wanacheza pamoja na mashabiki ambao wanajitokeza kuona burudani.

Ukweli ni kwamba wengi huwa wanatazama sehemu ya kukaa mashabiki pamoja na sehemu ya kubadilishia nguo na kuachana na habari za sehemu ya kuchezea.

Katika hili hapa ninaona kwamba ni makosa ambayo yanafanyika kwa sababu ambazo ninashindwa kuzielewa lakini nina amini kwamba ikifanyiwa kazi kwa ukaribu majibu yatapatikana.

Ikiwa ligi ipo mzunguko wa pili taarifa zimetolewa na Bodi ya Ligi Tanzania,(TPLB) kwamba kuna baadhi ya viwanja vimefungiwa kwa matumizi ili kuboreshwa.

Katika hili ninapenda kutoa pongezi kwa Bodi ya Ligi kwa kufungia baadhi ya viwanja kwa kile ambacho kimeelezwa kuwa ni kutokuwa bora hasa sehemu ya kuchezea (pitch).

Uwanja wa Gwambina ile ya Mwanza na Uwanja wa Karume unaotumiwa na Biashara United ya Mara nao pia umekutana na rungu kwa kufungiwa.

Kufungiwa kwa viwanja hivi nina amini kwamba ni hatua nzuri hasa katika maboresho ya kazi kwa wachezaji pamoja na ushindani kuwa imara.

SOMA NA HII  YANGA YAFICHUA SIRI YA USHINDI KWA ALLIANCE

Matokeo ndani ya uwanja yanapatikana ikiwa sehemu ya kuchezea itakuwa bora na kila mmoja atacheza kwa kujiamini tofauti na viwanja vingine ambavyo havikuwa bora.

 Ikiwa viwanja vingine vipo na havina ubora ninashauri vifungiwe ili vifanyiwe maboresho na yakitokea haya mafanikio makubwa yataonekana hapo baadaye.  

Tumekuwa tukilalamika kwa muda mrefu kuhusu viwanja na ubora wa sehemu za kuchezea kwa baadhi ya sehemu ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara.

Muda mwingi kuhusu sehemu ya kuchezea wengi wamekuwa wakitazama na kuboresha sehemu za kukaa mashabiki pamoja na vyumba vya kubadilishia nguo.

Watu kuwekeza nguvu kubwa sehemu ya kukaa halafu sehemu ya pitch kuiweka kiporo ilikuwa inaumiza hasa kwa wale ambao wanaingia uwanjani kusaka ushindi.

Mfano mzuri tuliona kwenye Uwanja wa Nelson Mandela uliochezwa fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba na Namungo FC kule Sumbawanga.

Mchezo ulikosa ile ladha halisi ya ushindani kwa kuwa sehemu ya kuchezea ilikuwa mbovu na wachezaji walishindwa kuonyesha yale makeke ambayo wanayo katika kutoa burudani.

Kwa kuwa hatua zimeanza kuchukuliwa imani yangu ni kwamba itakuwa endelevu na kwa wale ambao watashindwa kutimiza majukumu yao basi sheria na ifuate mkondo wake.

Ikumbukwe kuwa kulikuwa na utaratibu wa ukaguzi kabla ya ligi kuanza kwa kuwa wengi walikuwa wanaanza kufanya hivyo kisha ripoti inatolewa na vile viwanja ambavyo vitapitishwa ndivyo vilikuwa vinatumiwa.

Sasa hapa ndipo sielewi msimu huu mambo yamekuwaje kwa viwanja kupitishwa ama suala la ukaguzi lilikuajekuaje? Bado sijaelewa mpaka sasa namna hali ilivyokuwa.

Nani aliweza kufanya ukaguzi kwa wakati ule, sijajua labda hapa wahusika wenyewe wataweza kutusaidia ili kujua msimu huu mambo yalikwendaje kuhusu wakaguzi?

Hapo pana maswali kidogo kwa kuwa kama vilikaguliwa na wataalamu kutoka kwenye mamlaka sasa ilikuaje vikapitishwa kwa ajili ya matumizi ndani ya ligi?

Mpaka mechi mbili zimechezwa ndo wanafunga maana  timu zote zimecheza tayari na viwanja vimetumika.

Ni Biashara United walicheza mechi mbili ila Gwambina FC wao walicheza mechi moja kisha taarifa zikatolewa na maamuzi yakawa namna hiyo kwa kuwa wenye mamlaka imeamua.

Kikubwa kinachotakiwa katika hili ni kuona kwamba kila mmoja anaweza kufikia malengo lakini asiwepo yule wa kumrudisha nyuma mwingine lazima uwajibikaji uendelee ndani ya kile ambacho wanakifanya.

Imani yangu ni kwamba kila mmoja kwa sasa ambaye amepewa majukumu ya kuboresha viwanja atasimamia pale ambapo amepewa kazi yake.

Wale ambao watakuwa ndani ni lazima kuangalia kwa ajili ya wakati ujao na muhimu kila mmoja akatimiza majukumu yake kwa wakati. Mambo bado kufikia pale ambapo tunahitaji ila muhimu viwanja vyote vikakaguliwa.