Home Uncategorized MFEREJI HUU NDIO CHANZO CHA KUPIGWA CHINI ZLATKO, UNAPASWA UZIBWE

MFEREJI HUU NDIO CHANZO CHA KUPIGWA CHINI ZLATKO, UNAPASWA UZIBWE


 KUNA kauli kadhaa zimekuwa zikitolewa na watu mbalimbali hasa makocha wa kigeni waliobahatika kufundisha soka hapa nchini wakisema kwamba, Watanzania wengi wanajifanya makocha na kukusoa hata pasipohitaji kukosolewa.

 

Kauli hiyo unaweza kusema ni kama ya utani, lakini ina ukweli ndani yake kwa sababu makocha wengi wanapata shida, si wazawa wala wa kigeni.

 

Kufundisha soka ni kazi kubwa sana, makocha wengi wanapitia wakati mgumu hasa wanapopanga kikosi kwa ajili ya mechi, wakati mwingine hata kwenye kufanya usajili.

 

Ukiangalia usajili uliofanywa na timu kadhaa za hapa nyumbani kabla ya kuanza kwa msimu huu, wapo ambao walikosoa, pia walipongeza kwa baadhi ya sajili. Lakini kubwa zaidi ni kwenye kukosoa.

 

Kukosoa huko kumekuwa kukiendelea kila kukicha. Hata viongozi wa klabu nao wanakumbana na changamoto hiyo hasa pale wanapomleta kocha ambaye kwa muda mfupi anaonekana hafai mbele za macho ya watu.

 

Kulikuwa na kelele za chini kwa chini juu ya aliyekuwa  Kocha Mkuu wa Yanga, Zlatko Krmpotic kwamba hafai kutokana na aina ya ufundishaji wake ndani ya timu.

Hapo ndipo ambapo unaweza kuangalia ni wapi ambapo kulikuwa kunapitisha hizo kelele za chinichini, mfereji wa makosa ya kujirudia na kuanza kuvurugana unaaswa uzibwe ili kuleta maendeleo ndani ya soka la Bongo.


Mvurugano unapoanza mapema mwisho huwa hauwi mzuri kwa sababu kila mmoja atakuja na mbinu zake ambazo zinaweza kuchukua muda mrefu kuzoeleka.


Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi kwenye mahojiano yake alikuwa anasema kwamba kupata matokeo ya mabao finyu sababu ilitokana na maandalizi ya muda mfupi.


Hivyo hapo ndipo pa kupatazama vizuri hata kwa yule ajaye pia isije kuwa mwendo ni uleule wa zile kelele.

Licha ya kwamba timu ilikuwa inashinda, lakini haichezi soka la kuvutia. Hapa mashabiki wanataka kuona soka la kuvutia, hawajali sana matokeo. Hii inashangaza kweli.

 Na tayari ameshafungashiwa virago huku sababu ikiwa haijawekwa wazi. Ni maisha ya soka namna yalivyo na hamna namna lazima maisha yaendelee kwa kuwa wamekubaliana wenyewe.

SOMA NA HII  WACHEZAJI SIMBA WAGOMA KISA MPUNGA

Kuna wakati unaweza kukuta timu inacheza vizuri, lakini suala la matokeo linakuwa mtihani kwao. Nawakumbusha kidogo ilivyokuwa kwa Arsenal chini ya Kocha Arsene Wenger. Kuna kipindi ilikuwa inacheza soka la kuvutia, lakini haina mafanikio.

 

Kikubwa hadi sasa mashabiki wengi huwezi kufahamu wanataka nini hasa. Unaweza kuifanya timu icheze vizuri, wakakupigia kelele wanataka ushindi.

 

Ukianza kucheza soka la kusaka ushindi, utaambiwa tunataka na burudani. Ukiviweka vyote kwa pamoja, watakuja na sera kwamba tunataka mchezaji acheze. Ilimradi wakutikise tu.

 

Nimeanzia mbali lakini pointi yangu kubwa ni kwamba, kikosi cha Taifa Stars kimetangazwa, wapo ambao wameanza kuwanyooshea vidole wachezaji waliochaguliwa na Kocha Mkuu, Ettiene Ndayiragije.

 

Tunatakiwa tufahamu kwamba Taifa Stars ni timu ya Watanzania wote, walioitwa tunatakiwa kuwapa sapoti inayotakiwa ili tu kuipa mafanikio timu.

 

Tukianza kuwabagua kwa kuwapa sapoti baadhi na wengine kuwatenga, hatutakuwa na timu bora kwa sababu wachache wataingia unyonge na kushindwa kupambana.

 

Taifa Stars inapokwenda kucheza mechi ya kirafiki, ndiyo muda sahihi wa kuwatazama wachezaji wetu wote kabla ya kufika mechi za kimashindano.

 

Mechi hizi za kirafiki huwekwa kwa lengo la kuviweka sawa vikosi vyetu. Linapokuja suala la mashindano, huo ni wakati wa kushindana na si kujaribu wachezaji.

 

Tumuachie kocha afanye kazi yake ipasavyo, tusijifanye makocha wakati hatuna taaluma hiyo na hata kama unayo, mwachie aliyepewa dhamana ya kuiongoza timu husika.

 

Ni wazi binadamu kila mmoja ana mawazo na maono yake, ukiangalia Tanzania ina wachezaji wengi tena wa viwango vya juu, tunatakiwa kumuachia kocha anapowachagua wachache, tuwaunge mkono.

 

Kila la heri Taifa Stars katika maandalizi yenu kuelekea mechi hiyo ya kirafiki, kufanya kwenu vizuri ndiyo maandalizi bora kuelekea michezo ya kufuzu Afcon na Kombe la Dunia kwa wakati mwingine.