Home Uncategorized KMC TAYARI KWA MCHEZO WA KESHO, KOMBE LA SHIRIKISHO

KMC TAYARI KWA MCHEZO WA KESHO, KOMBE LA SHIRIKISHO


KIKOSI cha KMC FC kesho Mei Mosi kitashuka katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa ajili ya mchezo wa michuano ya Kombe la Shirikisho ( ASFC) dhidi ya Dodoma Jiji FC mchezo ambao utapigwa saa 10:00 jioni.

Kocha msaidizi wa KMC, Habibu Kondo amesema kuwa tayari walishafanya maandalizi ya kutosha tangu wakiwa jijini Dar es Salaam na kwamba hana hofu katika mchezo huo licha ya kwamba michuano hiyo ni migumu lakini anakiamini kikosi chake kitakwenda kufanya vizuri na hivyo kuendelea katika hatua inayofuata ya michuano hiyo ya ASFC.


Ameongeza kuwa timu anayokutana nayo kesho ni nzuri na kwamba imekuwa ikifanya vizuri katika michezo yake ya ligi kuu hivyo pamoja na yote bado kama kocha na benchi la ufundi kwa ujumla watahakikisha kuwa Kino Boys inakwenda kufanya vizuri katika mchezo wa kesho.


“Michuano hii inafahamika kabisa kwamba ukifungwa unatoka, kwahiyo pamoja na kwamba tunakutana na timu yenye ushindani mkubwa, lakini KMC FC imejiandaa vizuri kwa sababu tunahitaji kuchukua kombe hilo awamu hii, na uwezo huo tunao” amesema Habibu Kondo.


KMC inakutana kwa mara ya pili na Dodoma Jiji ambao katika mchezo wa kwanza ulikuwa ni wa ligi ambapo walicheza katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na Kino Boys kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.


SOMA NA HII  VITA YA MAPINDUZI LEO NI SIMBA AMA MTIBWA KUJULIKANA