Home Habari za Simba Leo AZIM DEWJI AUSHAURI UONGOZI WA SIMBA…UBORA WA YANGA

AZIM DEWJI AUSHAURI UONGOZI WA SIMBA…UBORA WA YANGA

Azam Dewji simba

BOSI wa zamani wa Simba, Azim Dewji amewatuliza mashabiki huku akiwaomba Mohammed Dewji na Mwenyekiti wa Bodi, Salim Abdallah Mhene ‘Try Again’ kujitokeza hadharani kusema jambo.

MO Dewji ambaye alikuwepo Simba ikicheza fainali pekee ya CAF kwa klabu hiyo amesema kwa hali ilivyo sasa MO na Try again mmoja wao anatakiwa kutoka hadharani na kutuliza upepo kwa wanachama na mashabiki wao ili kelele zitulie.

Bilionea huyo, alisema kilichoiponza Simba msimu huu ni kuimarika kwa wapinzani wao wakubwa kwenye ligi Yanga na Azam ambao walikuwa na vikosi bora zaidi.

“Simba sio mbovu kama ambavyo wengi wanaona, shida kubwa hapa ni ubora ambao wanao Yanga na Azam kwasasa wakati kikosi chetu kikiwa na mapungufu machache yanayotokana na ubora,”alisema Dewji.

“Simba ili itoke hapa kwanza viongozi wetu wanatakiwa kutoka hadharani na kuongea na mashabiki wao ikibidi hata kuitisha mkutano, baada ya hapo wawaeleze mipango yao ya kuitoa timu hapa ilipofika watu wataelewa na huo mkakati ukafanye kazi kwelikweli.

“Hakuna mwekezaji ambaye atatoa fedha za kununua wachezaji akavumilia kuona usajili unaofanyika haukidhi viwango, kama kuna changamoto za ubora wa wachezaji wakati huu viongozi wahakikishe hayo hayajirudii, pia mashabiki wanatakiwa kuelewa sio kila mchezaji akisajiliwa basi atafanya vizuri kwa haraka kama ambavyo alikuwa kule anakotoka.

“Tumeona kwa Fredy (Kouablan) alivyokuja hakuwa na kasi ambayo tuliitarajia lakini hapa mwisho ameonyesha kitu kikubwa, hata Fei Toto (Feisal Salum) alipoanza pale Azam hakuwa na makubwa ila baadaye akashika kasi kubwa.

“Mashabiki wetu wanatakiwa kutulia kuwasubiri viongozi watakuja na lipi kwa msimu ujao, tuache kila mtu kuwasema vibaya viongozi hadharani, hili litatubomoa zaidi badalka ya kutujenga.

“Kuna watu naona wanataka mambo ya kufukuzana, mimi binafsi siungi mkono sana hili, tutaendelea kuvurugana, kama kuna viongozi wataona wameshindwa kuendana na kasi ya mahitaji ya timu wakiamua kwa hiari yao kujiuzulu ni sawa lakini isiwe kwa shinikizo kama wachache wanavyofanya,”alisisitiza.

Dewji alisema Simba hawatakiwi kusajili idadi kubwa ya wachezaji ili kupunguza gharama kwa kuwa Simba bado ina wachezaji wazuri wanaohitaji muda huku akitaka kama kutakuwa na mchakato wa kusaka kocha mpya aje wa kukaa muda mrefu.

“Eneo ambalo tunakosea sana ni kusajili wachezaji wengi unaweza kuwa na kikosi cha wachezaji 25 tu na ukafanya vizuri, hapa utapunguza gharama za kuitunza timu yako lakini pia kama wakitafutwa kila nafasi wachezaji wawili bora wakawa wanashindana timu itaimarika.

“Nasikia anatafutwa kocha mpya, tunatakiwa kubadilika tuachane na makocha wanaokaa muda mfupi, hili ndio linafanya kila wakati tunasajili hovyo kwa kuwa kila kocha ana mahitaji yake, tuangalie kwa Yanga walikuwa na yule Nabi (Nasredine) alikaa pale miaka miwili akapata mafanikio, akaja huyu Gamondi (Miguel) naye atakaa miaka miwili anapata mafanikio.

“Azam nao walikuwa kama sisi lakini wakashtuka, wameshakaa na kocha wao huyu (Yusuf Dabo) kwa mwaka mmoja wameanza kubadilika na sisi Simba tujitathmini shida yetu iko wapi mpaka makocha hawataki kukaa kwa muda mrefu?,”aliongeza.

SOMA NA HII  WAKALA WA MPANZU AFUNGUKA KILICHOKWAMISHA...USAJILI WA MTEJA WAKE SIMBA