Home Habari za Simba Leo VITA KALI SIMBA…LAMECK LAWI & YUSUPH KAGOMA WAHUSIKA

VITA KALI SIMBA…LAMECK LAWI & YUSUPH KAGOMA WAHUSIKA

Habari za Simba Leo

Lameck Lawi na Yusuph Kagoma wana vita ngumu iliyowashinda wazawa wengi ndani ya kikosi cha Simba kwa misimu mingi mfululizo, wachezaji hao wameshamwaga wino na kinachosubiriwa ni kutangazwa rasmi.

Hata hivyo Afisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema klabu yake inatamani kuwa na wachezaji hao wawili kwa vile wana viwango vizuri na wanaweza kuwa msaada ikiwa wataichezea msimu ujao.

“Yusuph Kagoma ni mchezaji mzuri, ni mchezaji wa maana sana. Sisi tuliwapoteza Jonas Mkude na Thadeo Lwanga, kwa hiyo kama tutampata wanasimba tutafurahi sana kwa sababu tutaenda kutibu tatizo letu, lakini kwa sasa Kagoma ni mchezaji wa Singida Fountain Gate.

Lameck Lawi ni kijana mwenye kipaji cha hali ya juu na ana umri mdogo. Amekuwa akicheza vizuri na tayari amekuwa akicheza kwenye timu ya taifa. Sidhani kama leo hii kuna timu haitamani kuwa na mchezaji wa aina yake,” alisema Ahmed Ally.

Lawi anajiunga na Simba akitokea Coastal Union ambayo tayari ameshaiaga katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu msimu uliomalizika dhidi ya KMC wakati Kagoma amesajiliwa na Simba akitokea Singida Fountain Gate.

Mtihani mkubwa kwa wawili hao ni kupenya mbele ya wachezaji wa kigeni na kuingia katika kikosi cha kwanza ingawa wazawa wanaowakuta kikosini huenda wasiwe kikwazo kikubwa kwao.

Ugumu zaidi unaonekana utakuwa kwa Lawi ambaye katika nafasi ya beki wa kati ya Simba, wageni wamekuwa wakicheza mara kwa mara huku mara chache sana fursa hiyo ikienda kwa wazawa.

Katika msimu uliomalizika, Simba iliwatumia Enock Inonga na Che Fondoh Malone na baada ya Inonga kuumia ndipo Kennedy Juma akapata nafasi ya kutosha ya kucheza.

Inaonekana kama Simba itasajili beki mwingine wa kati ikiwa Inonga ataondoka ili aweze kucheza sambamba na Malone, hivyo anaweza kuwa kikwazo kwa Lawi kujihakikishia nafasi ya kudumu kikosini.

Hata hivyo Lawi ana nafasi kubwa ya kuwa chaguo la kwanza la beki wa kati mzawa mbele ya Kennedy Juma na Hussein Kazi ambao viwango vyao katika msimu uliomalizika havikuridhisha wengi.

Uwepo wa Fabrice Ngoma na Boubacar Sarr, unampa kibarua kigumu Kagoma kupenya na kuingia katika kikosi cha kwanza cha Simba ingawa pia kama Sadio Kanoute asipoondoka, vita ya namba inaweza kuwa ngumu zaidi kwa kiungo huyo aliyenaswa kutoka Singida Fountain Gate.

Kanoute, Ngoma na Sarr ndio wamekuwa kipaumbele cha benchi la ufundi la Simba katika kucheza nafasi ya kiungo wa ulinzi kwenye msimu uliomalizika huku wazawa wawili, Mzamiru Yassin na Hamis Abdallah wakisotea benchi katika michezo mingi.

SOMA NA HII  YANGA HUKO NI KAZI KAZI HAINA KUPOA