Home Habari za Simba Leo MAKOCHA, WACHEZAJI, WACHAMBUZI WATOA NENO USAJILI WA SIMBA…AHOU VS CHAMA

MAKOCHA, WACHEZAJI, WACHAMBUZI WATOA NENO USAJILI WA SIMBA…AHOU VS CHAMA

Habari za Simba, Ahoua vs Chama

WADAU wa Soka mbalimbali  wakiwemo  makocha wa Zamani  wa Simba,  wachezaji na wachambuzi wameonekana kutupia jicho zaidi  kwenye sajili za Simba, huku kubwa zaidi ni usajili wa Jean Ahoua na kuondoka kwa Clatous Chama kujiunga na Yanga.

Kocha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema Chama ni mmoja tu na pengo lake haliwezi kuzibika, lakini lazima aisha yaendelee kwani sio wa kwanza kuondoka Simba.

“Simba inasajili mchezaji sio kwa ajili ya kuwa kama aliyeondoka. Ilishawahi kuwa na wachezaji bora wakaondoka lakini wakaja wengine na kufanya vizuri. Walikuwepo kina Abdallah Kibadeni, Athuman Idd  Machuppa, Yusuf Macho, Emmanuel Okwi wakaondoka na timu ikasajili wengine.

Nadhani jambo la msingi ni wachezaji waliosajiliwa akiwemo huyo Ahoua kutimiza vyema majukumu yao uwanjani na baadaye nao wanaweza kujitengenezea ufalme wao kama kina Chama walivyofanya,” alisema Mwaisabula, huku kiungo wa zamani wa Simba, Abdulswamad Kassim aliongeza kwa kusema kwa muda aliokaa na Chama kikosini hapo haoni kama kuna mchezaji anaweza kuziba pengo hilo lakini akapendekeza kuaminiwa kwa walioopo nao wataisaidia Simba.

“Sijamuona Ahoua akicheza, lakini nimemuona Chama na nimecheza naye. Hakuna mtu wa kumfananisha naye. Anajua sana pia ana vitu vya kipekee ambavyo viungo wengi hawana. Lakini sio tatizo kwani kuna mechi nyingi tu Simba imecheza bila Chama na imeshinda hivyo naamini waliopo wakipewa muda na kuaminiwa wanaweza kufanya vizuri.

“Kikubwa ni timu kufika malengo na sio kumtegemea mchezaji mmoja tu,” alisema Abdul ambaye kwa sasa ni mchezaji huru.

Aliyewahi kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda alisema Chama ni mchezaji mzuri na amefanya makubwa ndani ya Simba, lakini ameondoka na timu hiyo inajipanga kucheza bila yeye.

“Chama ni mchezaji mzuri na mpira ndio kazi yake. Alifanya makubwa akiwa Simba, sasa ameondoka hivyo kwa sasa tunapanga mambo yetu kama Simba bila kumtegemea Chama. Hakuna mchezaji anayecheza milele kwenye timu hivyo kuondoka kwa Chama watakuja wengine na naamini watafanya vizuri,” alisema Mgunda.

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Amri Kiemba alisema mashabiki wa Simba hawapaswi kuishi na presha na matarajio makubwa kwa wachezaji wapya kwani ni msimu ambao timu hiyo imeamua kuanza upya hivyo wachezaji wanahitaji muda kuingia kwenye mifumo na kuelewana vyema.

“Matarajio hayapaswi kuwa makubwa sana kwenye msimu huu ambao timu imeanza kujitengeneza upya. Wasiwape presha sana wachezaji na kuwalinganisha na walioondoka kikubwa wajiandae kisaikolojia na wawape muda hata huyo Ahoua,” alisema Kiemba.

SOMA NA HII  SIMBA WARUDI NA MIL 600 TZ KUMPATA MPANZU