Home Habari za Simba Leo HATIMAYE ISRAEL MWENDA AINGIA KAMBINI…SHIDA IKO HAPA

HATIMAYE ISRAEL MWENDA AINGIA KAMBINI…SHIDA IKO HAPA

Habari za Simba- Mwenda

NYOTA mpya wa Singida Black Stars, Israel Mwenda amewasili rasmi ndani ya kikosi hicho baada ya hivi karibuni kuibuka mgogoro wa kimaslahi baina ya pande zote mbili zilizosababisha beki huyo kushindwa kuwasili kambini kwa muda muafaka, huku akikabiliwa na kazi nzito ya kuliamsha kikosini.

Mwenda aliyesajiliwa na Singida msimu huu akitokea Simba aliyoitumikia kwa misimu mitatu tangu mwaka 2021 akitokea KMC, alishindwa kujiunga na timu hiyo hadi alipolipwa Sh 60 milioni walizokubaliana katika mkataba baina ya pande zote mbili.

Wakati nyota huyo anamkimbia Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliokuwa anapambana nao Simba, ila habari mbaya pia kwake anaenda Singida ambayo pia ina mabeki wakali wa kulia na kushoto ambao wanacheza pamoja nafasi moja.

Katika upande wa kulia ambao hucheza Mwenda atakutana na beki, Ande Koffi Cirille aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast ambaye tayari ameonyesha uwezo mkubwa katika michezo yote miwili aliyocheza.

Cirille tayari ameonyesha ni beki anayeweza kukaba na kushambulia kwani amedhihirisha hilo wakati wa mchezo wa kwanza wa kikosi hicho dhidi ya KenGold uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya ambao Singida ilishinda kwa mabao 3-1, Agosti 18.

Katika mchezo huo, Cirille alichangia bao moja kati ya hayo ‘Assisti’ aliyoitoa kwa Elvis Rupia aliyefunga la pili kwa kichwa baada ya beki huyo kutoka na mpira kuanzia pembeni mwa uwanja huo na kuingia hadi ndani kisha kupiga krosi nzuri.

Upande mwingine ambao Mwenda anacheza ni beki ya kushoto ambao pia ndani ya kikosi cha Singida amesajiliwa mmoja kati ya mabeki bora na wenye uzoefu mkubwa Mghana, Ibrahim Imoro aliyejiunga nayo msimu huu akitokea timu ya Al Hilal ya Sudan.

Mbali na Imoro ambaye ni mchezaji wa kigeni ila Mwenda atakutana pia na ushindani mkubwa kwa wachezaji wenzake wazawa kwani katika mabeki wa kushoto wapo pia, Yahya Mbegu aliyetokea Fountain Gate FC na Edward Manyama aliyetoka Azam FC.

Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Patrick Aussems alisema, katika timu yoyote ili uweze kushinda mataji mbalimbali ni lazima utengeneze kwanza kikosi cha ushindani, hivyo suala la nyota wanaocheza nafasi zaidi ya moja kwake anajivunia.

“Kwa msimu mzima tunacheza zaidi ya michezo 30, huwezi kujihakikishia hakuna mchezaji atakayepata majeraha ingawa ukiwa na wachezaji wengi wanaocheza nafasi zaidi ya moja kwa ufasaha hata benchi la ufundi linajivunia, kwetu ni jambo nzuri.”

SOMA NA HII  STRAIKA LA MABAO SIMBA QUEENS AGOMBANIWA ULAYA...MWENYEWE KAANIKA HAYA...