Home Habari za Simba Leo SIMBA YAWAFUATA AL AHLI…MAMBO MATATU YA FAIDA KWAO

SIMBA YAWAFUATA AL AHLI…MAMBO MATATU YA FAIDA KWAO

Habari za Simba leo

Timu ya Simba inatarajiwa kushuka uwanjani Jumapili hii kwenye mchezo wa kwanza wa raundi  ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa nchini Libya dhidi ya Al Ahli Tripoli.

Al Ahli inakutana na Simba baada ya kuiondosha Uhamiaji ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 5-1, ambapo mchezo wa kwanza ilishinda mabao 2-0 kabla ya mechi ya pili kupata ushindi wa mabao 3-1 mechi zote zikipigwa Libya.

Simba inaanza kucheza raundi ya kwanza kutokana na kuwa juu kwenye viwango vya soka Afrika ikiwa inashika nafasi ya saba huku Al Ahli Tripoli ikishika nafasi ya 33 Afrika.

Hata hivyo, kuna sababu kadhaa ambazo zinaifanya mechi hiyo kuonekana kuwa upande wa Simba zaidi, kuliko vijana hao wa Libya ambao kwa hivi karibuni hawana rekodi kubwa zaidi kwenye soka Afrika.

Majeruhi

Mlinda mlango namba moja wa klabu ya Al Ahli, Mohammad Nashnoush (36) yupo nje ya uwanja akiuguza majeraha ya goti, hivyo atawakosa Simba katika michezo yote miwili.

Nashnoush ambaye ni kipa mzoefu sana akiwa amecheza michezo mingi kwenye mashindano ya kimataifa nafasi yake itachukuliwa na kipa namba mbili Suleiman Al Tihar (22), ambaye si mzoefu katika mechi za kimataifa ambapo amecheza mechi mbili tu dhidi ya Uhamiaji ya Zanzibar akiruhusu bao moja.

Wastani wa umri

Simba imefanya usajili wa wachezaji wengi wenye umri chini ya miaka 25, kama Joshua Mutale, Edwin Balua, Valentin Nouma, Jean Ahoua,Steven Mukwala, Valentino Mashaka na Leonel Ateba ambao wanacheza mpira wa kasi kuelekea lango la timu pinzani.

Al Ahli ina wachezaji wengi wenye umri mkubwa ambao wanaweza wasimudu kasi ya wachezaji wa Simba, wakongwe waliopo ni kama Mohammed Al Munir (32), Sanad Al Werfalli (32), Ahmed El Trbi (32), Thierry Manzi (28), Bakhit Khamis (30), Abdullah Al Sharif (28), Mourad Hedhli (33), Ahmed Krawaa (35), Ali Bouargoub (32), Agostinho Mabululu (32) na Abdllah Al Orfey (30), wakati wachezaji wengine wana wastani wa miaka 22-27, huku wanaoanza wengi ni wenye miaka 27-35.

Viwango vya CAF

Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Klabu ya Simba inashika nafasi ya saba ikiwa na alama 39, wakati Al Ahli Tripoli ikiwa nafasi ya 33, hivyo kwenye takwimu za makaratasi Simba inaonekana kuwa na kiwango cha juu zaidi ukilinganisha na wapinzani wanaokwenda kukutana nao.

Simba ambayo inaondoka kesho alfajiri inakwenda kwenye mchezo huu ikiwa imefanya maandalizi mazuri ambapo imecheza michezo miwili ya kirafiki mmoja dhidi ya Al Hilal ya Sudan ikitoa sare ya 1-1, mchezo mwingine dhidi JKT Tanzania ikishinda mabao 2-0.

SOMA NA HII  SIKU CHACHE BAADA YA KUTIMULIWA SIMBA...PABLO KAANIKA KILA KITU WAZI...KATAJA WACHEZAJI WALIOMCHOMESHA....