Home Uncategorized KARIA AITAJA SERIKALI KUHUSU HATMA YA LIGI KUU

KARIA AITAJA SERIKALI KUHUSU HATMA YA LIGI KUU

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kuendelea kwa Ligi Kuu na ligi nyingine kutategemea maelekezo ya Serikali kuhusu usalama na tahadhari ya ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Serikali ilizuia shughuli zote za mikusanyiko ikiwamo za kimichezo kwa siku 30 kuanzia Machi 17 ikiwa ni kuchukua tahadhari ya mlipuko wa ugonjwa wa corona unaotikisa dunia.

Wakati zikisalia siku sita kukamilika kwa tarehe hiyo iliyotangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Karia alisema mechi za ligi hazitaendelea baada ya kipindi hicho hadi watakapopewa maelekezo ya kufanya hivyo kutoka serikalini.

Hivi karibuni Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), lilitaka wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni kutoondoka kwenye timu zao hadi pale ligi ya nchi husika itakapomalizika, waraka ambao Karia amesema unaeleweka.

“Hali halisi inaonekana, kwenye Ligi yetu hakuna mchakato wowote unaoendelea hadi pale Serikali itakapotoa maelekezo,” alisema.

Licha ya hivi karibuni baadhi ya wadau kushauri Ligi Kuu ifutwe na wengine kutaka ichezwe bila mashabiki kipindi hiki cha tahadhari ya corona, Karia alisema hayo ni mawazo yao na si msimamo wa TFF.

SOMA NA HII  YANGA WAANZA KUIVUTIA KASI TANZANIA PRISONS