Home Uncategorized KASSIM DEWJI AWEKA HADHARANI WALICHOIFANYA ZAMALEK CAF 2003

KASSIM DEWJI AWEKA HADHARANI WALICHOIFANYA ZAMALEK CAF 2003

ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Dewji ‘KD”, ameweka wazi timu hiyo ilifanya vema katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye msimu wa 2003 kwa sababu walikuwa na kikosi bora kilichokuwa na wachezaji waliojitolea katika kiwango cha juu.

Msimu huo Simba ilitinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa kuwaondoa waliokuwa mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri.

Kassim aliliambia gazeti la NIPASHE kuwa, Simba ilifanya vizuri katika michuano hiyo kwa sababu ya hatua za awali kupangwa na timu ndogo ambazo zilisaidia kuwajengea uzoefu wachezaji wao.

“Sisi tulianza katika utaratibu mdogo, sababu tulianza na timu za kawaida mno, tulikwenda Botswana tukashinda, tukacheza na Santos, tukasonga mbele kwa penalti hapa Dar es Salaam, tukapiga penalti 12, tukawatoa penalti 13 ndio tukawatoa,” alisema Kassim.

Katibu huyo aliitaja mechi dhidi ya Zamalek ilikuwa na ‘mitihani’ kutokana na mazingira ya wakati huo lakini faida ya bao 1-0 waliloshinda katika mechi ya kwanza hapa nyumbani iliwaweka katika nafasi nzuri kwenye mchezo wa marudiano.

Alisema Simba ilikuwa na sehemu nzuri ya ufundi ambayo iliongozwa na marehemu Mkenya James Siang’a, na kupata ushirikiano kutoka kwa makocha wengine waliokuwa wanaishi Oman akiwamo, Talib Hilal.

“Kikosi kile kilikuwa ni kikosi madhubuti, siwezi kukisahau,…katikati nilikuwa na wigo mpana sana, nilikuwa na Gabriel (Emmanuel), Machupa (Athumani), Nteze (John), Mzee wa Kiminyio (Madaraka Selemani), lakini pia faida kubwa niliyokuwa nayo katika kiungo cha juu, nilikuwa na Yusuph Macho, Wilfred Keto, Shekhan Rashid, walikuwa viungo wengi sana, viungo wale walikuwa na uwezo wa kuisaidia timu kwenda mbele na kupata matokeo,” Kassim alisema.

Aliongeza kuwa wachezaji wa sasa hawachezi kwa kujituma hali ambayo inasababisha timu kutolewa mapema kwenye michuano.

“Enzi zile hatukuwa na mishahara mikubwa, mchezaji alikuwa analipwa Sh. 120,000, lakini fedha za bonasi zilikaribia Sh. milioni 2, ilisaidia kuongeza hamasa kwa kila mmoja wao,” alisema kiongozi huyo.

SOMA NA HII  MASTAA SIMBA WAMTEGA ROBERTINHO

Aliongeza anatarajia kukiandaa kikosi hicho kilichoitoa Zamalek chini ya nahodha Selemani Matola kucheza mechi ya utangulizi katika Tamasha la Simba Day litakalofanyika mwaka huu.