Home Uncategorized YANGA BILA TSHISHIMBI, KWA SIMBA KUTAKUWA NA TATIZO…

YANGA BILA TSHISHIMBI, KWA SIMBA KUTAKUWA NA TATIZO…


Na Saleh Ally
SIMBA na Yanga sasa zitakutana tena Julai 12, ikiwa ni mara ya tatu katika mwaka huu, tayari gumzo la watani limeanza.

Gumzo lenyewe ni kukutana kwa watani hao safari hii ikiwa katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.


Atakayepata ushindi katika mechi hiyo atapata nafasi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho ambalo bingwa wake atakuwa mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa.


Yanga lengo lao ni kuchukua Kombe la Shirikisho ili kupata nafasi moja iliyobaki ya michuano ya kimataifa. Simba wanataka nafasi hiyo kwa ajili ya rekodi na heshima kwa kuwa tayari wamepata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kupitia ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
  
Gumzo kwa sasa ni kukutana kwa Yanga na Simba na linakuwa ni gumzo linalofanana na magumzo mawili yaliyopita ya msimu huu wa 2019-2020.


Mangumzo hayo yalitokea katika mechi zote mbili za Ligi Kuu Bara ambazo ziliishia kwa Yanga kutoka sare na baadaye kushinda, hivyo kukusanya pointi nne katika mechi mbili huku Simba ikiambulia moja.

Mashabiki wa Yanga sasa hiyo ndiyo silaha yao kuu katika utani, kwamba wanakubali watani wao pamoja na kuonekana ni bora zaidi yao, lakini hawafui dafu wanapokutana nao.


Wakati yanaanza magumzo hayo ilikuwa hivi, mechi ya kwanza, Simba wakajigamba na kueleza namna walivyo bora kuliko Yanga na adhabu kali watatoa. Kitakwimu huu ni uhalisia, lakini kama nilivyowahi kuandika makala kuwa kila dakika 90 ya watani wa jadi inajitegemea sana. Mechi ikaisha kwa sare ya mabao 2-2.


Simba ndio hawakuamini, kama unakumbuka walitangulia kufunga mabao 2-0, lakini Yanga wakachomoa na kuwapa wakati mgumu kwelikweli. Baada ya hapo, gumzo likahamia katika mechi ya pili.


Yanga nao wakaanza tambo na kusema wanawaweza Simba, Simba wakaanza kuhoji Yanga walitokaje katika mechi hiyo na wasubiri mechi ya pili.


Ilipowadia ikaisha kwa Simba kupoteza kwa bao 1-0 huku Yanga wakionyesha soka safi sana. Simba hawakuwa tena na la kusema na waliona hakukuwa na nafasi ya kukutana na Yanga msimu huu.
Ukimya ukatawala, kukawa hakuna ujanja zaidi ya kusubiri msimu ujao. Lakini bahati nzuri sasa wanakwenda kukutana tena kwa mara ya tatu ndani ya msimu mmoja, mara ya tatu kwa mwaka wa 2020, kazi ipo.


Hakuna ubishi Simba ina timu bora zaidi ya Yanga hata ukichukia aina ya mchezaji mmojammoja. Lakini lazima tukubali, Yanga wanapokutana na Simba, huwa wanabadilika sana.


Moja ya sehemu ambayo Yanga wamekuwa wakionyesha mfano wa kuigwa ni namna ambavyo huwa wanajituma vilivyo. Wanapambana hasa na unaona ni wale waliopania hasa kushinda dhidi ya Simba.


Upambanaji wa Yanga, ndio umechangia wao kupata sare, umechangia wao kushinda mechi ya pili, jambo ambalo bila shaka kwa kuwa wanajua ni mtoano watafanya hivyo pia katika mechi ya Julai 12.

Wakati wakifikiria kufanya hivyo, basi wajipange vilivyo katika eneo la kiungo kwa kuwa ubora wa Simba ni katikati ya uwanja kutokana na kuwa na viungo mahiri sana. Wengi wao ni wazoefu, wenye vipaji na uwezo mkubwa.


Kama Yanga watacheza bila ya nahodha wao, Papy Tshishimbi, basi wajue kutakuwa na tatizo kubwa. Mfano mechi waliyoshinda kwa bao 1-0, uliona namna Tshishimbi alivyofanya kazi kubwa ya kuiongoza Yanga kuanzisha na kupeleka mashambulizi mbele.


Kocha Luc Eymael alifanya kazi kubwa ya kusimamisha kiungo baada ya kuweka viungo watatu waliokuwa wakicheza kama duara. Yaani Tshishimbi, Fei Toto na Haruna Niyonzima na hii ikawasumbua sana Simba.


Kama Yanga watavunja ile duara waliyoitumia katika mechi iliyopita, bila shaka watakuwa katika matatizo makubwa dhidi ya Simba siku hiyo.


Kuna taarifa ambazo si rasmi, kwamba kuna tatizo la mkataba na Tshishimbi, ingawa inaelezwa ni majeraha tu yanamsumbua. Kuna taarifa kiungo wake, Issa Mohammed Banka naye ana matatizo ya mkataba, ninaamini wanaweza wakayamaliza na kufanya mambo yaende vizuri. Lakini ni lazima wawe imara katika sehemu ya kiungo ambako ndiko nguvu ya Simba ilipo.


Kama Simba wakifanikiwa kukukamata katika kiungo na ukawa dhaifu, basi ijue hakuna namna zaidi ya kusubiri kipigo na kwa mechi ya watani, presha ikiwa kubwa, unaweza kujikuta unaingia katika stress ya kupigwa bao nyingi. 

SOMA NA HII  SIMBA YATUMA SALAMU KWA MTIBWA SUGAR