Home Habari za Simba Leo TAJIRI AS VITA AINGILIA DILI LA MPANZU SIMBA…TRY AGAIN ATUA DR CONGO

TAJIRI AS VITA AINGILIA DILI LA MPANZU SIMBA…TRY AGAIN ATUA DR CONGO

Habari za Simba- Elie Mpanzu

RAIS wa Klabu ya AS Vita, Amadou Diaby amekutana na winga wa kikosi hicho, Elie Mpanzu Kibisawala ili kumshawishi aendelee kubaki ndani ya timu hiyo baada ya hivi karibuni kuhusishwa kuhitajika na miamba wa soka nchini, Simba.

Winga huyo ni miongoni mwa wachezaji wanaohitajika na Simba katika dirisha hili la usajili ili kuboresha kikosi hicho ambacho kinajengwa upya ili kuleta ushindani msimu ujao baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo.

Taarifa kutoka DR Congo zinaeleza kwamba, Mpanzu ameshawaaga wachezaji wa timu hiyo huku akiwaambia anataka kupata changamoto sehemu nyingine jambo ambalo limemfanya Amadou kufanya kikao cha siri na mchezaji huyo.

Katika kikao hicho inaelezwa hawajafikia muafaka wa kile anachotaka mchezaji huyo, huku ofa aliyowekewa na timu yake ikiwa ni kubwa kuliko ya Simba japo mchezaji mwenyewe ameonyesha utayari wa kuondoka ili kutafuta changamoto sehemu nyingine nje ya mji wa Kinshasa.

Taarifa tulizozipata zinaeleza kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba ambaye kwa sasa ni mjumbe baada ya kujiuzulu nafasi hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ yupo DR Congo kwa mazungumzo.

“Ni kweli Try Again yupo Congo, lakini siwezi kusema kwamba ameenda kwa ajili ya dili hilo kwa sababu huwa ni mtu ambaye anaenda nchi mbalimbali kwa mambo yake binafsi. Kama ni hivyo sawa ila siwezi kukuhakikishia,” kimesema chanzo kutoka ndani ya Simba.

Hivi karibuni Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally wakati wa maswali na majibu katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram alipoulizwa kuhusu usajili wa Mpanzu, alisema wamemuona winga huyo kuwa ni mchezaji mzuri ila hawezi kuweka wazi kama wamemsajili.

“Hili ni dirisha la usajili na mengi yanazungumzwa. Nikisema nizungumzie kila mchezaji anayetajwa kutua Simba nitachoka. Naomba hili tuliache kwanza kwani muda wa kutambulisha wachezaji tuliowasajili ukifika tutafanya hivyo,” alisema Ahmed.

Hata hivyo, wakati AS Vita ikihaha kubaki na nyota huyo, lakini uongozi wa timu hiyo tayari umeanza kutafuta mbadala wake huku ikielezwa inahitaji kumrejesha aliyekuwa winga wa kikosi hicho, Marouf Tchakei.

SOMA NA HII  POWER DYNAMO WALIFICHA SILAHA ZAO HAPA KUHUSU SIMBA

AS Vita inapiga hesabu za kumrudisha Tchakei ambaye kabla ya kutua nchini alitokea timu hiyo na kujiunga na Singida Big Stars na baadaye Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars kuanzia Julai Mosi, mwaka jana.