Home Habari za Simba Leo KWANINI COASTAL WANAGOMBANA NA SIMBA? UNAKUMBUKA KISA CHA VIATU VYA NAVY?

KWANINI COASTAL WANAGOMBANA NA SIMBA? UNAKUMBUKA KISA CHA VIATU VYA NAVY?

Habari za Simba, LAMECK LAWI

Ugomvi wa Coastal Union na Simba haujaanza juzi tu kwenye sakata la Lameck Lawi bali umeanza miaka mingi iliypita, na kinachofanya Vilabu hivi viwili kongwe kuwa na utemi na ugomvi, ni mgongano wa kimamlaka.

Simba iliitaka huduma ya beki huyo wa Coastal Union na kufuata taratibu zote, wakakubaliwa.

Ikatakiwa ilipe kiasi fulani cha fedha kama ada ya uhamisho, ikakubali. Wakapewa tarehe ya mwisho ya kukamilisha malipo, wakakubali.

Lakini bahati mbaya kwao ni kwamba ikashindwa kufanya kama walivyokubaliana, yaani kulipa ada ya uhamisho ndani ya muda waliokubaliana.

Coastal Union ikasitisha biashara, Simba ikakurupuka na kwenda kulipa kile kiasi Coastal Union wakakataa.

Simba wakaingia mtandaoni na kumtambulisha mchezaji kama ni wa kwao Coastal Union wakabisha, bonge moja la sinema.

Huu ni mvutano mmoja katika mivutano mingi baina ya timu hizi mbili zenye historia ya udugu.

Kiasili Simba SC na Coastal Union SC zina vinasaba vya udugu.

Kabla ya kuitwa Simba SC, klabu hiyo iliitwa Sunderland iliyokuwa timu ya vijana wazawa wa Dar es Salaam.

Baadaye ikaungana na Arab Sports, timu ya watu wenye asili ya Kiarabu waliokuwa wakiishi Dar es Salaam.

Hiyo pia ndiyo historia ya Coastal Union vilabu kadhaa vya soka vya wazawa wa ukanda wa Pwani wa Tanga, viliungana na kuunda timu moja, ndiyo hii Coastal Union, yaani Muungano wa Pwani.

Coastal Union ikaungana na Arab Boys, timu ya Waarabu wa Tanga.

Inasemekana Waarabu hawa wa Tanga na wale wa Dar es Salaam walikuwa na uhusiano wa karibu sana na uhusiano huo ndiyo udugu baina ya vilabu hivi viwili.

Yawezekana historia hii haijanyooka barabara, lakini kimsingi ni kwamba vilabu hivi vina vinasaba vya udugu.

Simba ilianzishwa mwaka 1936 na Coastal Union ikaanzishwa miaka 12 baadaye, yaani 1948.

Miaka yote ya 1950 hadi 1960, timu hizi ziliishi kama ndugu.

Uharibifu ulianza miaka ya 1970 na kuendelea miaka yote ya 1980, 1990, 2000, 2010 na hata mwanzoni mwa 2020 hadi sasa unapokuja uhamisho wa Lameck Lawi.

Zifuatazo ni baadhi ya sababu za ugomvi baina ya ndugu hawa.

1. JENGO LA COASTAL UNION

Mnamo miaka ya 1970, Coastal Union walitaka kujenga ofisi zao mpya pale barabara ya 11 kata ya Ngamiani mjini Tanga.

Wakawaomba Simba waende Tanga kucheza mechi ya kirafiki na Coastal Union ili kuchangia ujenzi.

Simba walikataa. Coastal Union wakawaomba Yanga, wakakubali tena kwa kujilipia kila kitu kwenye hiyo safari ya Tanga.

Faida yake ndiyo hilo jengo ambalo hadi sasa ndiyo makao makuu ya Coastal Union.

Kitendo cha Simba kukataa kiliwauma sana Coastal Union ambao waliamini ilikuwa haki yao kuisaidiwa na ndugu zao wa damu.

2. VIATU VYA NAVY

Miaka ya 1970, chama cha soka Tanzania, FAT, kilikumbwa na hali mbaya sana ya kiuchumi iliyosababisba madeni mengi.

Mwaka 1975 chama hicho kikapata Mwenyekiti mpya, mwanasheria mahiri Said El Maamry ambaye sasa ni marehemu.

El Maamry akaenda kwa Rais wa nchi, Julius Nyerere (naye merehemu), kuomba msaada wa kifedha ili kupunguza madeni.

Nyerere akamjibu kwamba hata serikali haina pesa kwa hiyo akitaka aandae mashindano maalumu ili kuisaidia kukusanya pesa.

Ndipo mwaka 1976 yanaandaliwa mashindano yaliyoitwa OFUMA CUP, yaani Kombe la OFUMA.

OFUMA maana yake ilikuwa Operesheni Futa Madeni.

Timu nyingi zilishiriki, wakiwemo Coastal Union, Pan Africa ambao ndiyo walianzishwa tu mwaka huo, Simba na Navy kutoka Zanzibar. Hao Navy kwa sasa ndiyo KMKM.

Simba wakiwa wamesahau walichowafanyia Coastal Union kwenye ujenzi wa jengo, wakawakaribisha kukaa palepale klabuni kwao Msimbazi wakati jengo bado jipya tu.

Coastal Union wakakubali lakini moyoni mwao bado walikuwa na kinyongo kikubwa sana na walipanga kulipa kisasi.

Mashindano yaliendeshwa kwa kuhesabu alama, mwenye nyingi ndiyo bingwa.

Coastal Union walimaliza mechi zao dhidi ya Navy na kushinda japo Navy ndiyo walipewa nafasi kubwa sana kutwaa mashindano kutokana na umahiri wao wa kusakata kandanda.

Baada ya mechi, Navy wakawazawadia Coastal Union viatu vyao walivyochezea mechi vilikuwa vipya kabisa.

Simba walikuwa wanamalizia mechi yao siku iliyofuata, dhidi ya Pan Africa.

Wakishinda watakuwa mabingwa, kinyume na hapo, Coastal Union mabingwa.

Ili kuwaharibia Simba, Coastal Union wakawapa Pan Africa vile viatu walivyopewa na Navy ili wavae dhidi ya Simba.

Na kweli, Pan Africa wakavaa vile viatu na kukamua kweli kweli…Simba haikushinda mechi na akaukosoa ubingwa.

Walikasirika kuona timu waliyoipokea kama ndugu imewahujumu kwa kuwapa wapinzani wao viatu.

Kwa Coastal Union ilikuwa kicheko mara mbili, kwanza wamelipa kisasi na pili wametwaa ubingwa.

3. MKASA WA FURA MWEKALO

Kulikuwa na mchezaji aliyeitwa Francis Mwekalo. Aliichezea Coastal Union mwaka 1986 kisha mwaka huohuo akaenda Simba na akacheza, lakini alijibadili jina na kujiita Fura Mwekalo.

Mwisho wa msimu Simba waliongoza ligi na walistahili kuwa mabingwa.

Lakini Coastal Union wakakata rufaa FAT, BMT, kwa Waziri wa michezo na kisha mahakamani kupinga Simba kumtumia mchezaji huyo ambaye alikuwa wa kwao.

Coastal Union ikataka ipewe alama ambazo Simba walipata dhidi yao kwa sababu mchezaji huyo alicheza.

Mahakama ya hakimu mkazi Kisutu ikaamuru kwamba Fura Mwekalo na Francis Mwekalo ni mtu mmoja na alikuwa mchezaji halali wa Coastal Union.

Simba wakanyang’anywa alama na kuwaachia Tukuyu Stars ubingwa.

Coastal Union wakapewa zile alama na kuwanusuru kushuka daraja…bila hivyo wangeshuka.

Hii kitu Simba iliwauma sana…kwa Coastal ikawa furaha mara mbili; kuepuka kushuka daraja na kulipa kisasi cha kukatakiwa mechi ya ujenzi wa jengo.

4. ABDI BANDA

Mwaka 2014, Simba ilimchukua kitemi mchezaji chipukizi wa Coastal Union, Abdi Banda.

Simba walipewa taarifa za kikachero kwamba Coastal Union hawakumlipa mshahara wa miezi miwili mchezaji huyo.

Wakamwambia asichukue mwezi unaofuata ili iwe mitatu ambayo kisheria inatosha mchezaji kuvunjia mkataba.

Wakati huo Coastal Union walikuwa wanalipia mishahara ‘dirishani’. Banda akiwa na maelekezo ya wakubwa wa Dar, hakwenda kuchukua mshahara wake wa mwezi uliofuata.

Baadaye akasema hakulipwa miezi mitatu kwa hiyo anaondoka klabuni hapo.

Hii kitu Coastal Union iliwauma sana kwani huyo ndiye kijana wao wa Tanga na hawakutegemea awafanyie hivyo.

Lakini baadaye wakagundua mchezo mzima kwamba Simba walishaanza kumlipa mshahara tangu ile miezi miwili ya kwanza ambayo wao hawakumlipa…wakaumia zaidi.

CHUKI INAENDELEA

Mambo yote haya yakaweka mlima wa chuki na hasira kwenye nyoyo na vifua vya watu wa Coastal Union dhidi ya Simba.

Kilichofuata baada ya hapo ni mguu wa shingo mguu wa roho, kisasi juu ya kisasi.

5 MWAMNYETO

Simba walimtaka sana Bakari Nondo Mwamnyeto wa Coastal Union aende kwao. Lakini masharti ya Coastal Union yakaonekana makubwa sana kwa Simba.

Coastal Union walitaka wapewe udhamini wa shilingi 180 milioni kwa miaka mitatu na pesa taslimu milioni 30 kama ada ya uhamisho ya mlinzi huyo.

Simba wakaona hizo pesa ni nyingi sana, wakasusa…Yanga wakatoa na kumchukua mchezaji huyo.

Simba walikasirika sana na kupania kuwashusha daraja wagekapokutana kwenye ligi.

Itakumbukwa Coastal Union walikuwa kwenye hali mbaya sana na walitakiwa kukutana na Simba katika mechi za mwisho mwisho mwa msimu.

Siku ya mechi Simba ambao tayari wakishachukua ubingwa, wakaupiga mwingi ili kulipa kisasi.

Bahati mbaya washika vibendera hawakuwa vizuri siku hiyo, waliamuru kuotea na kuinyima nafasi zaidi ya 10 za kufunga ikiwemo kukataa mabao ambayo yalikuwa sahihi.

Coastal Union angefungwa mabao mengi siku hiyo, wangezidiwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa na timu zilizoshuka…yaani wangeikosa hata play off…na hilo ndilo lilikuwa lengo la Simba, japo hawawezi kukiri.

6. ABDUL HAMIS SULEIMAN SOPU

Baada ya hatr trick kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga pale Arusha, Sopu aliibuka kuwa bidhaa inayotafutwa sana.

Yanga wakafika bei palepale uwanjani. Azam FC wakafika bei na Simba wakafika bei.

Lakini Yanga wakakosa maarifa ya kupenya na kufanikisha dili.

Simba walifanikiwa kuongea na Coastal Union wenyewe na kumalizana kila kitu.

Azam FC waliongea na Sopu mwenyewe na kumalizana naye kila kitu.

Hatua iliyofuata kwa Simba ilikuwa kuongea na mchezaji, na Azam kuongea na Coastal Union.

Siku chache zilizopita Simba walitoka kumnunua Victor Akpan kutoka Coastal Union lakini pesa waliyokubaliana walikuwa hawajamalizia.

Kwa hiyo Simba waliporudi tena kwa Coastal Union kumtaka Sopu, Costal Union wakaweka sharti kwamba hawataki kuongea na Simba hadi walipwe fedha zao za Akpan.

Wakati huo CEO wa Simba, Barbara Gonzale alikuwa Morocco kwenye mkutano wa CAF, hela za klabu haziwezi kupatikana hadi CEO awepo.

Basi waliokuwepo wakaingia kazini kuitafuta pesa ya watu ili wafanikishe dili jipya.

Kumbe hadi wakati huo Azam FC ambao walikuwa chaguo cha mchezjai, wakawa wameshakubaliana na Coastal Union na Sopu ameshasaini.

Wakaombwa wasitangaze kwanza hadi watakapoambiwa kwa sababu wanasubiriwa Simba waweke pesa.

Saa nane mchana Simba wakaingiza pesa kwenye akaunti ya Coastal Union na hapo hapo Coastal Union wakawaambia Azam FC wamtangaze…wakamtangaza.

Hii sinema iliwauma sana Simba kwani waliona wamechezewa mchezo wa kitoto.

7. HATIMAYE KWA LAMECK LAWI

Kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu cha historia ya Yanga, Juni 15, 2024, Rais wa TFF, Wallace Karia, alikumbushia hasira za watu wa Coastal Union dhidi ya Simba SC zilizoanzia kwenye mechi ya harambee ya ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Coastal Union.

Siku chache baadaye linaibuka sakata la Lameck Lawi.

Ukisoma mstari kwa mstari kwenye kauli ya Karia, utaona kabisa kwamba hakuna upendo kati ya Simba na Coastal Union.

Coastal Union bado wana hasira sana na Simba na wanaamini bado hawajalipa kisasi cha kukataliwa mechi ya ujenzi wa jengo.

Kwa hiyo hata wanapokaa chini kuongea biashara ya mchezaji yoyote, wanaongea kwa sababu inabidi tu waongee.

Lakini pakitokea nafasi yoyote ya kuwaumiza wataitumia ili kulipa kisasi…ndicho kilichotokea kwa Sopu na Lawi.

Credit: Mwanaspoti

SOMA NA HII  NYIE HANGIKENI TU...LAMECK LAWI HUYOO KATUA ULAYA